Home Mchanganyiko WAZIRI LUGOLA KUANZA ZIARA MIKOA YA RUVUMA, MTWARA NA LINDI, KESHO JANUARI...

WAZIRI LUGOLA KUANZA ZIARA MIKOA YA RUVUMA, MTWARA NA LINDI, KESHO JANUARI 9, AWATAKA WANANCHI WAMLETEE KERO MIKUTANO

0

************************************

Na Mwandishi Wetu, MOHA, Dodoma.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola anatarajia kuanza ziara Januari 9, 2020, katika Mkoa Ruvuma, Mtwara na Lindi kufuatilia masuala ya ulinzi na usalama pamoja na maagizo mbalimbali aliyoyatoa kwa vyombo vilivyopo ndani ya Wizara yake.

Waziri Lugola ataanza ziara hiyo Januari 9, 2020 Mjini Songea Mkoani Ruvuma, Januari 10 Mjini Mtwara na Januari 11 Mjini Lindi, ambapo katika kila Mkoa atapokelewa na mwenyeji wake ambaye ni Mkuu wa Mkoa na kukutana na Wajumbe wa Kamati
ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii, akiwa njiani kuelekea
Mkoani Ruvuma, leo, Waziri Lugola alisema katika kila mkoa
atafanya mkutano wa hadhara, hivyo anawataka wananchi
wenye kero waje kwa wingi ili waweze kutatuliwa kero zao.

“Lengo la ziara hii ni kufuatilia utendaji kazi wa Taasisi zilizopo
ndani ya Wizara yangu, na pia kuzungumza na wananchi katika
mikutano ya hadhara, ikiwa ni utaratibu ambao nilijiwekea
tangu nilipoteuliwa kuiongoza Wizara hii,” alisema Lugola.

Alisema ziara hiyo pia itamwezesha kufuatilia kwa ukaribu zaidi
maagizo yake aliyoyatoa kwa vyombo vya ulinzi na usalama
ambayo ni dhamana zitolewe saa 24 katika vituo vyote vya
polisi nchini, na pia alipiga marufuku tabia ya baadhi ya Polisi
kubambikizia kesi wananchi, na pamoja na agizo la pikipiki zote
zilizopo vituoni ziondolewe.

“Nitafanya mkutano mkubwa wa hadhara katika Mji wa
Songea, Mtwara na Lindi, utaanza saa 10:00 hadi 12:00 jioni, hivyo nawaomba wananchi wa miji hiyo wajitokeze kwa wingi
kunisikiliza kile ambacho nimepanga kuwaambia, na pia
nitawapa nafasi wananchi waulize maswali bila woga, waniambie kero zao nami nitazitatua katika mkutano huo,”
alisema Lugola.

Lugola alisema katika ziara yake aliyoifanya Mikoa ya Kigoma, Kagera, Arusha, Morogoro, Katavi na Rukwa, amegundua wananchi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali hivyo hawezi kulala akiwa ofisini, lazima afanye ziara nchi nzima kuwasaidia wananchi kutatua kero zao ambapo wengi wao wakiwalalamikia na baadhi ya Polisi wakiwaonea.

“Napenda kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika mikutano yangu hiyo, wanapojitokeza itasaidia kusikiliza matatizo yao yanayowakabili, ndio mana nimepanga kufanya ziara kama hizi nchi nzima, hii inasaidia sana kujua matatizo mbalimbali ya wananchi pamoja na kuangalia utendaji kazi wa Taasisi zangu zilizopo ndani ya Wizara hii,” alisema Lugola.

Aliongeza kuwa, Serikali ya Rais Dkt. John Magufuli inawajali wananchi wake ndiyo mana inawafuata mahali walipo, ili wazungumze na Serikali yao uso kwa uso.

Waziri Lugola alisema katika Mikoa yote atakayoitembelea pia atazungumza na Watumishi rai ana askari waliopo ndani ya Wizara yake ambao ni Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Magereza, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, pamoja na Idara ya Probesheni ambayo jukumu lake kuu ni kupunguza msongamano gerezani na
kusimamia wafungwa waliopewa adhabu mbadala na
Mahakama au wafungwa waliopata msamaha.