Mmoja wa vijana wa chuo cha Lupyana Singida akitengeneza springi kwenye karakana ya ufundi magari katika chuo hicho.
Mazoezi kwa vitendo yakiendelea katika chuo hicho.
Mazoezi kwa vitendo yakiendelea katika chuo hicho.
Vijana wakiwa katika mazoezi ya vitendo katika chuo hicho.
Mazoezi kwa vitendo yakiendelea katika karakana ya magari kwenye chuo hicho.
ICT ni miongoni mwa kozi inayofundishwa chuoni hapo.
………………………………………………
Na Mwandishi Wetu, Singida
CHUO kipya cha Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi kinachojulikana kama ‘Lupyana Academy VTC’, kinatarajia mapema mwezi huu kuanza kutoa mafunzo mbalimbali ya ujuzi na stadi za kazi, katika kuwawezesha vijana mkoani hapa na mikoa jirani kuwa na nafasi nzuri ya wao kujiajiri na kuajiriwa, kulingana na mazingira yanayowazunguka
Taratibu zote za usajili wa chuo hicho kilichoanzishwa mwanzoni mwa mwaka huu zimekamilika, na kitaanza kutoa mafunzo hayo kulingana na mtaala wa Mamlaka ya Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini VETA, kwa idadi ya wanafunzi 20 kila kozi
Akizungumza kwenye eneo la Kindai, mkabala na Idara ya Maji na Bohari Kuu ya Mkoa, Manispaa ya Singida, ambako ndipo makao makuu ya chuo hicho, Msimamizi wa Chuo hicho, Mwalimu Wabeja Chubwa, alizitaja kozi zitakazofundishwa kuwa ni pamoja na ufundi wa magari, umeme, ujenzi, bomba za maji, udereva, ushonaji na ICT
Chubwa alisema kwa kuanzia azma ya chuo hicho ni kuhudumia jamii inayokizunguka chuo hicho, na baadaye wataendelea kupanuka maeneo mengine, huku wakiamini wanafunzi wengi baada ya kujiunga na hatimaye kuhitimu chuoni hapo watapata kitu cha kufanya badala ya kukaa bure mitaani
“Waombaji wote watarajie kuja kujifunza ufundi stahiki kulingana na mtaala uleule wa VETA, lakini tuna walimu wenye ubora na viwango vinavyokubalika, na walimu wote wamesajiliwa na mamlaka za juu,” alisema Chubwa
Alisema jina ‘Lupyana’ tafsiri yake ni ‘Neema,’ hivyo waasisi wa chuo hicho Enelisa Andengulile yeye ni niI Mhandisi wa Umeme na amekuwa akifundisha vyuo vya ufundi stadi kwa zaidi ya miaka 20 huku mwingine Edward Mgina yeye pia ni Mhandisi upande wa mitambo, na pia ni mwalimu wa ufundi stadi mwenye uzoefu mkubwa.
“Waasisi hawa katika utume na utumishi wao wameishi hapa Singida kwa muda mrefu, na hata wakistaafu maisha yao yatakuwa hapa hapa, hivyo kuanzisha chuo hiki ni kama sehemu ya shukrani zao kwa jamii ya wanasingida,” alisema Chubwa
Alisema Singida mbali ya VETA, vyuo vya ufundi stadi ni vichache sana, mathalani kwa mwaka uliopita vijana walioomba kujiunga na chuo cha Veta walikuwa 900, lakini waliobahatika kuchaguliwa ni vijana 100 pekee. Hivyo naamini chuo hiki kitakwenda kufungua milango hata kwa wale waliokosa nafasi ya kujiunga na Veta, kwa sababu kinafata misingi na kanuni za ufundishaji wa chuo cha Veta
Chubwa, ambaye pia ni mtaalamu wa somo la ICT ndani ya chuo cha Lupyana, alisema pamoja na kutangaza kuwa sifa ya kujiunga ni kuanzia darasa la saba na kuendelea, lakini miongoni mwa vijana wengi wanaoendelea kuleta maombi mpaka sasa ni wale waliohitimu vyuo vikuu mbalimbali nchini
Aidha, mbali ya vijana wa Singida, chuo hicho ambacho ni cha kutwa kinaendelea kupokea wanafunzi wa kozi hizo za ufundi stadi kutoka mikoa mingine ya Rukwa, Mwanza na Kigoma
“Tunaiomba serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo wawatumie vijana wanaopata mafunzo kwenye vyuo vya ndani ili kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ya Awamu ya Tano ya Ujenzi wa Viwanda, na hatimaye kulifikisha taifa hili kwenye uchumi wa kati kupitia nguvu kazi ya vijana wetu hawa, vijana wengi kwa sasa wanahitimu mafunzo yao wakiwa na ubora stahiki kulingana na mahitaji ya soko ikilinganishwa na huko nyuma“ alisema Chubwa