Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo pamoja na Makamanda wa Polisi pamoja na Kamati ya Usalama Mkoa wakifurahia Wimbo ambao Askari wa Jeshi la Polisi walikua wanaimba katika ufunguzi wa kikao kazi cha Makamanda wa Polisi Kanda ya Kaskazini kilichofanyika katika bwalo la Maofisa wa Polisi Mapema leo Jijini Arusha.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo (Katikati) akiwa amesimama pamoja na Makamanda wa Polisi pamoja na Kamati ya Usalama Mkoa wakati wimbo wa Jeshi la Polisi ukipigwa katika ufunguzi wa kikao kazi cha Makamanda wa Polisi Kanda ya Kaskazini kilichofanyika katika bwalo la Maofisa wa Polisi Mapema leo Jijini Arusha.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho gambo, Makamanda wa Polisi Kanda ya Kaskazini pamoja na Kamati ya Usalama Mkoa wa Arusha katika ufunguzi wa kikao kazi cha Makamanda wa Polisi kanda ya Kaskazini.
Maofisa na Askari wa Vyeo mbalimbali wakifuatilia kwa makini Maelekezo mbalimbali yaliyokua yanatolewa wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Makamanda wa Polisi Kanda ya Kaskazini kilichofanyika katika bwalo la Maofisa wa Polisi Mapema leo Jijini Arusha.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo akiongea na Makamanda wa Polisi Kanda ya Kaskazini pamoja na Maofisa, Wakaguzi na Askari wakati wa ufunguzi wa Kikao kazi cha Makamanda hao mapema leo Jijini Arusha.
……………..
Na Gasto Kwirini wa Jeshi la Polisi Arusha.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo amewataka Makamanda wa Polisi Kanda ya Kaskazini kuja na mikakati na mbinu za kisasa katika kukabiliana na matukio ya uhalifu.
Ameyasema hayo wakati akifungua Kikao kazi cha Makamanda wa Polisi kanda ya Kaskazini ambacho kinahusisha Mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara kilichofanyika mapema leo katika ukumbi wa bwalo la Maofisa wa Polisi Jijini Arusha.
Amesema pamoja na Jeshi hilo kufanya kazi nzuri, amewataka Makamanda hao kujadili na kuweka mikakati mipya na ya kisasa ambayo itawezesha katika kukabiliana na matukio ya uhalifu na wahalifu hususani mapambano dhidi ya madawa ya kulevya, Uhalifu unaovuka mipaka, Ulinzi wa Madini na kuweka mazingira mazuri ya kiusalama kwa sekta ya utalii.
‘‘Makamanda shirikishaneni mbinu za kisasa za kukabiliana na uhalifu, kwa sababu Wahalifu hawatakuwa na sehemu ya kukimbilia kwa kuzingatia maeneo yote katika kanda hii ya kaskazini mbinu za kihalifu zinafanana’’. Alisema Gambo.
Naye Kamishna wa Polisi Intelijensia ya Jinai CP. Charles Mkumbo ambaye pia ni Mlezi wa Kanda hiyo amesema lengo la kikao kazi hicho ni kuweka mikakati ya pamoja katika kuhakikisha Kanda hii inaendelea kuwa shwari hasa kwa kuzingatia kanda hii ni kitovu cha utalii hapa nchini.
‘‘Nimekuja ili kuhakikisha Makamanda hawa wanaungana pamoja, Kama ni msako ufanyike kwa siku moja katika mikoa yote ili kuhakikisha wahalifu wanakosa sehemu ya kujificha’’. Alisisitiza Kamishna Mkumbo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Makamanda wa Polisi Kanda ya Kaskazini ambaye pia ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga alisema wamekutana ikiwa ni utaratibu wao wa kukutana kila baada ya miezi mitatu kwa lengo la kubadilishana uzoefu wa kukabiliana na uhalifu.
Aliongeza kwa kusema kuwa watajadili na kuweka mikakati ambayo watakuja na maazimio ya pamoja ya kukabiliana na Matukio yote ya kihalifu hasa katika maeneo ya mipaka ya Namanga, Holili, Hororo na Tarakea ili kuhakikisha Wahalifu wanakosa sehemu ya kukimbilia.