Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amekipongeza Chuo cha Maendeleo Michezo cha Malya Kilichopo Wilayani Kwimba Mkoani Mwanza kwa kuendelea kuzalisha wataalam wa Tasnia ya Michezo hapa nchini ambapo amesema kutokana na umuhimu wa chuo hicho hapa nchini amemwagiza mkuu wa Chuo hichi, Bw.Richard Timothy Mganga kukifanya chuo hicho kuwa na uwezo wa kufanya utafiti wa kodi inayotokana na michezo mbalimbali inayofanyika nchini.
Dkt.Mwakyembe amesema hayo Disemba 12,2019 jijini Dodoma katika kikao kazi cha Maafisa michezo wa halmashauri na Mikoa Tanzania Bara chenye lengo la kutathimini, kujadili na kuelekezana namna bora ya kuimarisha michezo na kutumia sekta hiyo kutangaza vivutio vya utalii hapanchini.,ambapo amesema chuo hicho kimekuwa kinara katika utoaji wa elimu ya Michezo hivyo ni vyema pia kikajikita katika kufanya utafiti wa kodi inayotokana na Michezo inayofanyika hapa Tanzania.
Aidha,Dkt.Mwakyembe amewataka Maafisa Michezo kote nchini kulinda viwanja vya michezo na kutoa taarifa ya viwanja vya michezo vinavyobadilishwa hata kwa siri ili kujua ni namna gani Wizara yake iweze kushughulikia changamoto hiyo.
.
” Nataka niwaambie Wapo baadhi ya Wakuu wa shule na walimu wanaozuia michezo shuleni na mnawajua, mnakaa kimya sasa wajibu wenu ni nini? Tambueni michezo sasa ni ajira ambayo ni mgodi na taifa lina vijana wengi simamieni vyema michezo,” amesema.
Kwa Upande wake Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya Richard Timothy Mganga amepokea maelekezo hayo huku akisema baadhi ya changamoto zilizopo katika chuo hicho kuwa ni pamoja na Kutokuwa na Miundombinu ya kutosheleza mahitaji ikiwemo viwanja bora vya kisasa vya michezo , na majengo mbalimbali,Uhaba wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia michezo ,Idadi ya wanachuo kutofikia lengo kutokana na utaratibu wa ruhusa ,Uwepo wa waombaji ambao hawajawahi kushiriki kwenye michezo .
Pia Bw.Mganga amesema Chuo kimedhamiria kutumia michezo kama fursa ya kutoa ajira pamoja na kufanya biashara. Hivyo kimelenga kuweka ubora kwenye mitaala inayotarajiwa kuhuishwa ili iwasaidie wahitimu kutekeleza azma hii, naimelenga kutoa elimu kwa kuzingatia mafunzo yenye ‘competency descriptors’, ‘enablers’ na ‘learning outcomes”
Katika hatua nyingine Bw.Mganga amesema Chuo kimeongeza mapato yake ya ndani kwa asilimia 36.7 kutoka kiasi cha Tsh 212,080,783.36. mwaka 2017/2018 mpaka Tsh 289,877,562.00 katika mwaka wa fedha 2018/2019.
Bw.Mganga ameendelea kufafanua kuwa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kimefanikiwa Kutoa wahitimu mbalimbali ambao wanatekeleza majukumu katika maeneo mbalimbali nchini, takriban wahitimu 373 wamepata mafunzo ya Diploma; wahitimu hao ni ,Maafisa michezo ,Waalimu wamichezo mashuleni ,Waalimu wa michezo katika timu mbalimbali ,Wakufunzi wa michezo katika vyuo ,Waamuzi wa michezo
Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kilianzishwa 1979 katika eneo la mikutano ya Machifu ,Eneo (ekari 160.36) ktk Mkoa wa Mwaza (Wilaya ya Kwimba ekari – 91.28) na Mkoa wa Simiyu (Wilaya ya Maswa – ekari 69.08)
Naye Kaimu Katibu Mkuu Dkt. Ally Possi amemwagiza Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Yusuph Singo kukakikisha kikao kazi hicho kinakuwa endelevu na kufanyika kila mwaka. Aidha, aandae utaratibu wa kuwa na vikao hivyo kikanda vikiwa na lengo la kuwaandaa vijana waweze kushiriki michezo mbalimbali kitaifa na kimataifa.
“Kikao Kazi hiki kitatoa tathimini ya wapi tulipo, nini kifanyike pamoja na kutoa mwongozo wa kusimamia michezo mbalimbali na kutoa maelekezo kwa kuweka maazimio yatakayosaidia kupeleka michezo kuwanufaisha vijana maana michezo ni ajira,” alisema Dkt. Possi.
Aidha, Dkt. Possi aliwataka maafisa michezo hao kuzingatia mada ya uandishi wa maandiko ya udhamini katika michezo ambayo ni kichocheo cha kufanikisha michezo nchini kwani maandiko mradi hufanyika ni miongoni mwa kazi inayofanyika kila siku katika sekta ya michezo, hivyo ni vyema kuwa na ujuzi huo.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo nchini Yusuph Singo ametoa shukrani kwa Makatibu Tawala Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa na Halmashauri kwa kuwawezesha maafisa michezo hao kushiriki kikao hicho.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki wa kikao kazi hicho Afisa Michezo kutoka Wilaya ya Mbarali Bw. Gerald Chiwaya aliishukuru wizara kwa kuandaa kikao hicho ambacho kimefanyika kwa mara ya kwanza nchini ambacho kina washiriki 265 kutoka mikoa yote Tanzania Bara.
Kikao kazoo hicho Cha Maafisa Michezo kilianza Disemba 12,2019 na kikitarajiwa kuhitimishwa leo Disemba 13,2019.