***************************************
Viongozi wa Jumuiya ya Wazazi Chama cha Mapinduzi Taifa wakiongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Dkt. Edmund Mndolwa wametembelea Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa – SGR kipande cha Dar es Salaam – Morogoro eneo la Vingunguti hadi Stesheni jijini Dar es Salaam Novemba 28, 2019.
Viongozi hao wamefanya ziara hiyo kwa lengo la kuona maendeleo ya mradi, kujifunza pamoja na kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015/20 inayotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Katika ziara hiyo viongozi walipata fursa ya kuona kazi tofauti za Mradi wa SGR ambao kwa majumuisho zimefikia zaidi ya 72% kwa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro, sambamba na hayo walipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kungu Kadogosa kuhusu mabadiliko yanayoendelea kufanyika katika shirika ili kukidhi haja ya watanzania ya kupata usafiri wa uhakika na kufikia Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati.
Wakiwa katika eneo la Vingunguti viongozi wa Jumuiya ya Wazazi CCM walipata maelezo mafupi kuhusu Mradi kutoka kwa Mhandisi Ayubu Mdachi ambaye ni Meneja Mradi Msaidizi kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro ambaye amesema kuwa mradi umefika zaidi ya 72% huku zoezi la uwekaji wa miundombinu ya umeme ukiwa umefika 62%.
Akizungumza kwa niaba ya wenyeviti wa Mikoa, Mwenyekiti wa Jumuiya wa wazazi Mkoa wa Mwanza Ndugu Nyiliza Makongoro amesema kuwa wameridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo wa reli ambao unasimamiwa na wazawa kwa asilimia kubwa, pia wamewashukuru viongozi na wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania kwa kusimamia vyema mradi huo wenye maslahi kwa watanzania na taifa kwa ujumla.
Aidha Mkurugenzi Mkuu wa TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa aliwashukuru viongozi hao kwa kuutembelea Mradi wa SGR na kuwaambia kuwa TRC inatarajia kufungua njia ya Tanga hivi karibuni na safari inatarajiwa kuanza Desemba 6, 2019.
“Kwa niaba ya Serikali tunafungua reli ya kaskazini Daresalaam-Kilimanjaro kwa kuanza majaribio Tarehe 01 Desemba 2019, na tutaanza safari rasmi Tarehe 06 Desemba 2019, dhamira yetu ni kufika Arusha ambapo ukarabati wake mpaka sasa umefika zaidi ya 85%”.