Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Mst.) Harold Nsekela katikati akiwa katika
picha pamoja na Ujumbe kutoka Tume ya Maadili na Kupambana na
Ufisadiya Kenya iliyoongozwa na Kamishna wa Tume hiyo Bi Rose Mghoi
Macharia (kulia kwa Mhe. Nsekela) baada ya kuhitimisha ziara yao ya siku
tano katika Sekretarieti ya Maadili tarehe 22 Novemba, 2019 iliyokuwa na
lengo la kubadilishana uzoefu wa kiutendaji baina ya taasisi hizo mbili. (
Picha na Ally Mataula, Afisa Habari Sekretarieti ya Maadili)
Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Mst.) Harold Nsekela katikati na Watendaji
wengine wa Sekretarieti ya Maadili wakiwa katika picha pamoja na Ujumbe
kutoka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi ya Kenya iliyoongozwa
na Kamishna wa Tume hiyo Bi Rose Mghoi Macharia (kulia kwa Mhe.
Nsekela) baada ya kuhitimisha ziara yao ya siku tano katika Sekretarieti ya
Maadili tarehe 22 Novemba, 2019 iliyokuwa na lengo la kubadilishana
uzoefu wa kiutendaji baina ya taasisi hizo mbili. ( Picha na Ally Mataula,
Afisa Habari Sekretarieti ya Maadili)
*******************************************
Na. Ally Mataula.
Afisa Habari Sekretarieti ya Maadili.
Viongozi Waandamizi wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi kutoka nchini Kenya wamefanya ziara katika Ofisi za Sekretearieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Makao Makuu Jijini Dodoma.
Ziara hiyo ya siku tano iliyoanza tarehe 18 – 22 Novemba, 2019 iliongozwa na Kamishna wa Tume hiyo Bi Rose Mghoi Macharia ambaye alisema kuwa lengo la ziara hiyo ni kubadilishana uzoefu wa kiutendaji baina ya Tume hiyo na Sekretarieti ya Maadili.
Bi Macharia alisema kuwa wameamua kuja Tanzania kupata uzoefu katika suala la usimamizi wa Maadili kutokana na misingi imara iliyowekwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kuona kama kuna maeneo ambayo wanaweza kujifunza kutoka Tanzania.
Akielezea baadhi ya majukumu ya Taasisi yake, Bi Macharia aliyataja kuwa ni pamoja na kusimamia uzingatiaji wa Sura ya Sita na Ibara ya 151 ya Katiba ya Jamhuri ya Kenya, Kufanya uchunguzi na kutoa mapendekezo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka kushtaki kosa lolote linalohusu rushwa, uhujumu uchumi, vitendo vya ukiukaji wa misingi ya maadili na mambo mengine yaliyobainishwa na Sheria.
Shughuli nyingine ni Kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Maadili kwa Maafisa na Viongozi wa Umma, kupokea malalamiko yanayohusu ukiukwa wa Sheria ya Maadili unaofanywa na Maafisa wa Umma, Kufanya uhakiki wa uadilifu kwa watu wanatafuta nafasi ya kuteuliwa au kuchaguliwa kushika ofisi za umma, pamoja na kutoa elimu na uelewa kuhusu mambo ya mapambano dhidi ya rushwa na maadili nchini Kenya.
Akizungumzia kuhusu utaratibu wa kisheria wa Tanzania unaowataka Viongozi wa Umma kusaini Hati ya Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi wa Umma mara baada ya kuchaguliwa au kuteuliwa kushika nafasi katika Ofisi za Umma Bi Macharia alifurahishwa na utaratibu huo na kueleza kuwa unasaidia kuwakumbusha viongozi wakati wakitekeleza majukumu yao.
Naye Kamishna wa Maadili ambaye alikuwa ni mwenyeji wa ujumbe huo, alisema kuwa Sekretarieti ya Maadili ilianzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 132(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuchunguza tabia na mwenendo wa kiongozi wa umma yeyote kwa madhumuni ya kuhakikisha kwamba masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma yanazingatiwa ipasavyo.
Pia Mhe. Nsekela aliueleza ujumbe huo baadhi ya misingi ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inapaswa kuzingatiwa na Viongozi wa Umma wakati wakitekeleza majukumu yao. Aidha, kwa mujibu wa Mhe. Nsekela misingi hiyo inawataka watu wanaoshika nafasi fulani za madaraka kutoa mara kwa mara maelezo rasmi kuhusu mapato, rasilimali na madeni yao.
Pia, misingi ya maadili inapiga marufuku mienendo na tabia inayopelekea kiongozi kuonekana hana uaminifu, anapendelea au si muadilifu au inaelekea kukuza au kuchochea rushwa katika shughuli za umma au inahatarisha maslahi au ustawi wa jamii. Alifafanua Mhe. Nsekela.
Katika ziara hiyo ya siku tano, viongozi hao kutoka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi ya nchini Kenya waliweza kujifunza mambo mbalimbali kutoka Sekretarieti ya Maadili hususani katika maeneo kadha wa kadha ambayo ni pamoja na Mfumo wa Sera na Sheria inayokuza na kusimamia Maadili nchini, Taratibu za Kuanzisha, Kufanya Uchunguzi kuhusu ukiukaji wa maadili, njia ya kuwasilisha malalamiko na namna ya kusimamia Matamko ya Rasilimali za Viongozi wa umma.
Mambo mengine ni Uendeshaji wa Baraza la Maadili, usikilizaji wa malalamiko pamoja na utekelezaji wa adhabu kwa viongozi ambao wamebainika kukiuka Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Pia, Ujumbe huo ulipata fursa ya kujifunza Mifumo mbalimbali kama vile Mfumo wa Udhibiti wa Taarifa, Mfumo wa kielectroniki wa utoaji wa Matamko ambao upo katika hatua za mwisho kukamilika pamoja na Mfumo wa Ufuatiliaji wa Uzingatiaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Pamoja na kutembelea Sekretarieti ya Maadili, Ujumbe huo pia ulipata fursa ya kutembelea katika Taasisi nyingine za Umma ambazo ni Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, TAKUKURU, Chuo Kikuu cha Dodoma na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA).