Mwenyekiti wa CCM Wilayani Hanang’ Mkoani Manyara, Mathew Darema akikagua timu ya soka ya City Boys kabla ya mpambano na timu ya Young Boys kwenye uwanja wa shule ya sekondari Balang’dalalu.
Mwenyekiti wa CCM Wilayani Hanang’ Mathew Darema akikagua timu ya Young Boys.
………………………….
Mshindi wa tamasha la michezo Kata ya Balang’dalalu Wilayani Hanang’ Mkoani Manyara, ameshindwa kupatikana baada ya City Boys na Young Boys kufungana mabao 10-10 na kumalizika kutokana na giza.
Tamasha hilo liliandaliwa na Mwenyekiti wa jumuiya ya vijana wa CCM (UVCCM) kata ya Balang’dalalu, Emmanuel Gamasa lilifikia fainali jana na litarudiwa leo kwenye uwanja wa shule ya sekondari Balang’dalalu, baada ya bingwa kutopatikana.
Katika fainali hiyo hadi dakika 90 za mchezo huo zilipomalizika timu hizo za zilikuwa hazija fungana hivyo kulazimika kupigiana penalti tano kwa kila timu.
Wachezaji wa timu hizo walipigiana penalti tano kwa tano na kila moja wakakosa mabao mawili hivyo kuendelea kupiga wakiwemo magolikipa na kufungana mabao 10 -10 hadi giza likaingia na kuhitimisha mpambano huo.
Mgeni rasmi wa mpambano huo, Mathew Darema alizipongeza timu hizo na kuzipatia sh100,000 ili zigawane 50,000 kila moja baada ya kutopatikana mshindi.
“Fainali inabidi irudiwe kesho kwani giza limesababisha tukose uhondo nawazawadia sh100,000 kwa mchezo mzuri mgawane pia nitarudi kuona mchezo mwingine tupate bingwa” alisema Darema.
Mwenyekiti wa UVCCM kata ya Balang’dalalu, Emmanuel Gamasa alisema tamasha hilo limekuwa na mafanikio makubwa kutikana na hamasa kubwa ya jamii ya eneo hilo.
Gamasa alisema imedhihirika kuwa michezo ni furaha, amani na upendo ndiyo sababu watu wengi wamejitokeza kushuhudia pambano hilo.