Home Mchanganyiko KERO YA MIAKA 59 YA MAJI KITUO CHA AFYA NASSA YATATULIWA

KERO YA MIAKA 59 YA MAJI KITUO CHA AFYA NASSA YATATULIWA

0

Mkazi wa Kijiji ha Bukabile, Specioza Mahondola akitwishwa ndoo ya maji na Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwera baada ya kupokea mradi kisima cha maji uliojengwa na taasisi ya The Desk & Chair Foundation (TDCF).Kushoto anayehushudima ni mwenyekiti wa taasisi hiyo Sibtain Meghjee.

…………………………

 NA BALTAZAR MASHAKA, BUSEGA

TAASISI ya  The Desk & Chair Foundation imetumia sh.milioni 20 kutatua kero ya  maji  iliyodumu kwa miaka 59 ikiwakabili wananchi wa Kijiji cha Bukabile na Kituo cha Afya Nassa wilayani Busega katika Mkoa wa Simiyu.

Kisima hicho kirefu cha maji  kitatumiwa na wananchi wa kijiji hicho, wakiwemo wajawazito, wagonjwa wanaotibiwa na kulazwa kwenye kituo hicho cha afya  huku  taasisi hiyo ikitoa sh. 800,000 kugharamia vitambulisho vya wazee 800  vitakavyowatambulisha  kupata matibabu.

Mwenyekiti wa TDFC, Sibtain Meghjee, akikabidhi mradi huo kwa serikali, alisema  kisima hicho kirefu cha maji kimegharimu sh. milioni 20 na kimefungiwa pampu ya kusukuma maji  inayotumia nguvu ya umeme jua na hivyo kukiwezesha kituo cha Afya Nassa na wananchi kupata maji ya uhakika muda wote.

“Tumeridhishwa na mfumo wa mitambo iliyofungwa kisimani hapo kuwa inasukuma maji vizuri hadi kituoni baada ya majribio kufanyika.Kwa niaba ya wafadhili na uongozi wa The Desk & Cair Foundation, tunaikabidhi serikali mradi  huu, hatutakuwa na mamlaka nao isipokuwa kwa matengenezo ya mitambo itakapoharibika,”alisema.

Meghjee alisema taasisi hiyo imetekeleza miradi mbalimbali ya kijamii mkoani Simiyu ikiwa ni pamoja na kuboresha visima vifupi 11 vya maji na kuchimba vipya 12, kufunga mitambo ya umeme jua kwenye Kituo cha Afya Nassa, mradi wa maji safi na salama Lamadi, baiskeli 5 kwa walemavu wa viungo na moja ya kawaida.

Mingine ni mradi wa nyumba 10 za nyasi vijijini kufungiwa mfumo wa umeme jua,vyoo kwenye shule ya Malayele,vibebeo 300 kwa wajasiriamali na vitambulisho vya afya kwa wazee 800 huku miradi kama hiyo ikifanyika pia kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kati.

“Naishukuru serikali kwa kutoa vibali na ushirikiano wa dhatiwakati tunapotekeleza shughuli zetu kwa jamii katika maeneo mbalimbali ya nchi,kama ilivyo kauli mbiu yetu ya Tupo pamoja Iwe Dhiki Iwe Faraja:Huduma kwa Jamii Bila Kuchagua Bila Kubagua,”alisema Meghjee.

Aidha, baadhi ya akinamama wa Kijiji cha Bukabile ambao ni wanufaika wa mradi huo, Nadhifa Yusuf, Specioza Mahondola naWinfrida Masalu,walisema utainufaisha jamii na umewakomboa na adha ya kufuata maji  umbali mrefu,ambapo wakati wa kujifungua walipata shida ya kwenda na maji .

Walieleza kuwa wameteseka miaka mingi kufuata maji umbali wa km 4 kutokana na kijiji hicho kuwa mbali na Ziwa Victoria, walikuwa wakinunua maji sh.1000 kwa ndoo tano ama kuyateka kwenye madimbwi hivyo kwa sasa wataweza kushiriki shughuli za uzalishaji na maendeleo.

Kwa upande wa vitambulisho vya bima kwa wazee, mmoja wa wanufaika hao Kitula Kubangwa (71) aliishukuru The Desk & Chair Foundation kuwaondolea changamoto ya vitambulisho vya matibabu na kuishauri serikali iendelee kuwatizama kwa jicho la huruma.

Akipokea mradi huo Mkuu wa Wilaya ya Busega,Tano Mwera, alisema The Desk & Chair Foundation ni wadau wakubwa wa maendeleo kutokana na misaada yao kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha huduma mbalimbali kwa jamii.

Alisema mradi huo wa maji utabadilisha maisha ya wananchi na wagonjwa wanaotibiwa kwenye kituo cha afya Nassa kwani lengo la serikali ni kumtua mwanamke ndoo ya maji kichwani.

“Maji ni muhimu, mradi huu unaunga mkono juhudi za serikali za kuhudumia wananchi na kuwaletea maendeleo lakini pia sasa watayapata maji karibu na akinamama watatumia muda wao mwingi kufanya shughuli za maendeleo,”alisema Mwera.  

Awali Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Nassa, Fred Mruma, alisema changamoto ya maji tangu kujengwa kwa kituo hicho mwaka 1960 imekwisha ingawa bado wana tatizo la nishati ya umeme kwenye chumba cha upasuaji, mashine ya kufua nguo za wagonjwa na mashine ya kupima damu (Full Blood picture machine).