Na Dixon Busagaga ,Arusha .
KATIKA kuongeza thamani ya Utalii wa
milimani ,waongoza watalii zaidi ya 500 wa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro
wameanza kupatiwa mafunzo ya namna ya kutoa huduma ya kwanza kwa wageni pindi
wapatapo changamoto wakati wa kupanda.
Mafunzo hayo yanayofanyika kwa wiki
mbili kwa kuanza na jiji la Arusha yanatolewa bila malipo na kampuni ya
Utafutaji na Uokoaji ya Kilimanjaro SAR ya mkoani Kilimanjaro, mafunzo ambayo
hutolewa kipindi cha mapumziko ya biashara ya utalii.
Mtaalamu wa Masoko wa kampuuni hiyo ,William
Mbogo alisema Kilimanjaro SAR kwa miaka miwili ya mwanzo imeanza kutoa mafunzo
kwa waongoza watalii wa milimani peke yake na kwamba baadae watafanya kwa
waongoza watalii wa Safari za hifadhini.
“Kwenye mafunzo yetu haya
tumeyagawanya katika sehemu kuu tatu ,sehemu ya kwanza tuna wataalamu
wanaozungumzia namna ya kumpatia mtu huduma ya kwanza pale inapotokea mgeni amepata
changamoto ,hatuishii hapo tu wanaingia kufanya pia kwa vitendo.”alisema Mbogo.
Alisema sehemu ya pili ya mafunzo
hayo washiriki wanafundishwa namna ya kutambua aina mbalimbali ya magonjwa yatokanayo
na mlima na pia namna ya kumrejeshea uhai mtu ambaye amepatwa na tatizo la
upumuaji kwa kitaalamu wanaita CPR .
Mbogo alisema suala la usalama ni
kivutio kikubwa cha wageni kwa kampuni zinazofanya shughuli za utalii huku usalama
toa wito kwa kampuni hizo kuendelea kujenga imani na Kilimanjaro SAR ili kujiongezea
thamani katika biashara ya utalii .
“Sasa hivi kampuni za utalii zina ujasili wa kuuza mlima Kilimanjaro na Mlima
Meru wakijua kabisa kwamba kuna huduma ya haraka tena ya uhakika kwa kutumia helkopta
ambayo atapata mgeni wake na kampuni ya bima ya mgeni ndio itahusika kwenye
malipo”alisema Mbogo .
Naye Afisa Uhusiano na Masoko wa
kampuni ya Kilimanjaro SAR ,Abdulrahim Damian alisema kwa sasa mafunzo
yanatolewa kwa waongoza watalii pekee kwa sababu wao ndio viongozi wa kundi
linaloshiriki katika kuwapandisha wageni .
“Tunatoa mafunzo bure kwa hawa
waongoza watalii ambao tunaamini ndio viongozi ,tunawapa maarifa waweze
kuhudumia wageni lakini pia na watu wote ambao wanaongozana nao katika safari
ya kupanda mlimani “ alisema Damian.
“Hii tunafanya kwa sababu mbili, ya
kwanza tunashiriki katika uboreshaji wa huduma za kitalii hapa nchini kwa kushirikiana na wadu wote wa utalii
pamoja na serikali ili kuvutia wageni pindi wanapokuja nchini wasiwe na hofu
juu ya usalama wao.”aliongeza Damian.
Kwa upande wao washiriki wa mafunzo
hayo , Waongoza watalii ,Jonas Luta ,Joyce Jacob na Hussein Paul wameishukuru
Kampuni ya Kilimanjaro SAR kwa kuanzisha utaratibu wa kuwapa mafunzo hayo
ambayo wameeleza hawakuwahi kuyapata hapo awali .