Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (Kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (Kulia) baadhi ya vipeperushi vinavyoelezea sheria za watoto ili aweze kujielimisha zaidi ikiwa ni moja ya utamaduni wake kufanya hivyo anapofika katia ofisi za mihimili mingine ya serikali.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (Katikati) Katika picha ya pamoja na viongozi wa Mkoa (kuliani kwake) Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushotoni kwake) Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Mhe. David Mrango na viongozi wengine.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (Katikati) Katika picha ya pamoja na viongozi wa Mkoa (kuliani kwake) Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushotoni kwake) Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Mhe. David Mrangona viongozi wengine.
………………….
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameishauri Serikali kufanya tathmini ya kazi inayofanywa na wapelelezi pamoja na waendesha mashitaka katika kesi iwapo wanatekeleza wajibu wao ipasavyo.
Akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Joachim Wangabo alipomtembelea ofisini kwake akiwa katika ziara ya kikazi mkoani humo, Jaji Mkuu alisema Mahakama ya Tanzania inakabiliwa na changamoto ya kesi kutomalizika kwa wakati na wakati mwingine haki kutotendeka kutokana na wapelelezi pamoja na waendesha mashitaka kutotekeleza wajibu wao ipasavyo.
Aidha Jaji Mkuu ameishauri Serikali kuwabana wapelelezi na waendesha mashitaka ili wawe wanajiandaa vizuri katika kesi mbalimbali.
Alisema endapo kutakuwa na maandalizi hafifu ya hati ya mashitaka katika kesi huweza kusababisha upelelezi wa kesi hiyo kutofanyika inavyotakiwa na hivyo kupelekea wakati mwingine haki kutotendeka na kusababisha mfumo wa sheria kutoaminiwa na wananchi.
Alisema matumizi ya Tehama katika kesi yatarahisha na kusaidia haki kutendeka na kesi kumalizika kwa wakati huku akitolea mfano wa matumizi ya kipimo cha DNA kwenye kesi kubwa kama vile za mauaji na ubakaji. Alisisitiza umuhimu wa hivyo kuchukuliwa mapema kabla ya ushahidi haujapoa.
Akitolea mfano wa kesi kwenye Mahakama ya Rufani, Jaji Mkuu alisema wakati mwingine Majaji hukutana na changamoto ya maandalizi hafifu ya hati ya mashitaka kwa kuwa inakuwa haiendani na tukio lenyewe.
Alisema kutokana na kukua kwa sayansi na Teknolojia, hivi sasa wapelelezi hawana budi kuchukua maungamo ya kesi kwa njia ya picha video. “Upelelezi bado uko karne ya 16 wakati wahalifu wako karne ya 21”, alisema Jaji Mkuu.
Kuhusu Mahakama kuanza kutoa hukumu kwa lugha ya Kiswahili, Jaji Mkuu amesema suala hilo ni muhimu na Mahakama italifanyia kazi. Aliongeza kuwa hivi sasa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kinatoa mafunzo kwa Mahakimu ya uandishi wa hukumu kwa lugha nyepesi na inayoeleweka zaidi.
Awali akizungumza, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa aliiomba Mahakama kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha kesi zinamalizika kwa wakati hususani zile zinazohusiana na mimba za utotoni kwa wananfunzi wa shule za msingi pamoja na Sekondari zilizopo kwenye mkoa wake.
Alisema tayari kesi 40 za makossa hayo zimefikishwa mahakamani lakini kati ya hizo ni kesi tatu tu ambazo zimesikilizwa na kutolewa maamuzi. Alisema katika kipindi cha mwaka moja kanzia Julai 2018 mpaka Oktoba 2019 katika mkoa wake kuna jumla ya wanafunzi 294 waliopata mimba wakiwemo 209 wa shule za sekondari na 85 wa shule za msingi.
Naye Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Mhe. Halfan Haule aliiomba Mahakama kuangalia uwezekano wa kuanza kutoa hukumu kwa lugha ya kishwahili hasa kwenye ngazi ya Mahakama za wilaya ili kuwawezesha wananchi kuzielewa kwa urahisi.
Alisema hivi sasa wananchi walio wengi hutumia muda mwingi kuzunguka kwenye ofisi mbalimbali za wanansheria ili kupewa tafsiri za hukumu zao hatua inayowafanya kuchelewa kupata haki ikiwemo kuchelewa muda wa kukata rufaa endapo wanakuwa hawajaridhishwa na hukumu zilizotolewa.
Jaji Mkuu ameanza ziara ya kikazi Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Sumbawanga ambapo awali alikagua miradi ya ujenzi katika mkoa wa Songwe pamoja na kupokea taarifa ya utekelezaji ya Mahakama kuu kanda ya Sumbawanga. Jaji Mkuu anaendelea na ziara kukagua shughuli za Mahakama katika wilaya za Nkasi na Kalambo.
Na Lydia Churi-Mahakama Sumbawanga