Lina Ndemfoo akichapa kazi katika kiwanda cha TBL Arusha.
*********************************
Wakati bado kuna dhana kwenye jamii kuwa baadhi ya kazi ni maalumu kwa ajili ya Wanaume na kusababisha Wanawake wengi kuzikimbia, wapo baadhi ya Wanawake makini wanaamini kuwa kazi au taaluma zote zinahusu jinsia zote na wameweza kuthibitisha suala hilo kwa vitendo.
Miongoni mwao ni Lina Ndemfoo, Mhandisi wa mitambo katika kiwanda cha kutengeneza Bia cha TBL kilichopo mjini Arusha, ambaye pia anatoa wito kwa Wasichana waliopo mashuleni kuacha dhana ya kuogopa baadhi ya masomo hususani ya Sayansi na hesabu na kudhani kuwa hawayawezi
Katika mahojiano hivi karibuni Mhandisi, Lina Ndemfoo, alisema kuwa pamoja na majukumu mengi ya kazi aliyonayo huwa anahakikisha anasoma mambo mbalimbali kuhusiana ufundi wa mitambo na teknolojia mpya zinazoibuka kila kukicha duniani ili kuhakikisha anakwenda sambamba na mabadiliko hayo
“Naipenda taaluma yangu ya uhandisi wa mitambo, muda wangu mwingi huwa nautumia kusoma mambo mengi yanayohusiana na fani hii kwa kuwa teknolojia inakuwa kwa kasi kubwa kiasi kwamba, ukitaka kuwa mtaalamu na kufanya kazi kwa ufanisi kwenye kampuni kubwa kama TBL, unahitaji kuhakikisha muda wote unakwenda na wakati”, alisema Lina.
Alisema mara nyingi huwa anawaza ni jinsi gani wasomi wa fani ya sayansi nchini wanaweza kutumia taaluma zao kuleta mabadiliko kwenye jamii kupitia ubunifu wa kiteknojia badala ya kutegemea ubunifu wa wataalamu wa nje ya nchi.
Mhandisi Lina Ndemfoo, alisema kuwa amepata elimu ya Shahada ya kwanza ya Uhandisi wa Mitambo, katika chuo cha Dar es Salaam Institute of Technology (DIT) na alikuwa miongoni mwa wahitimu waliofanya vizuri katika mwaka wao wa 2017.
Baada ya kumaliza masomo aliajiriwa na Kampuni ya TBL, katika kiwanda cha Arusha, akiwa kama mwendeshaji mashine za uzalishaji. Kutokana na ufanisi wake katika kazi katika kipindi cha muda mfupi amepandishwa kufikia nafasi aliyonayo ya ufundi wa Mitambo.
Mbali na kupata elimu za vyuoni akiwa mwajiriwa wa TBL, tayari amehudhuria kozi mbalimbali za ndani ya kampuni ambazo zimezidi kumpatia maarifa katika fani yake na kumfanya awe na uwezo sambamba na kujiamini katika kuendesha na kuifanyia matengenezo mitambo iliyotengenezwa kwa teknolojia za kisasa.
“TBL kuna mafunzo ya aina nyingi na kuna mitambo ya kisasa na tumekuwa tukipata mafunzo ya aina mbalimbali ikiwemo ya mifumo ya uendeshaji viwanda kwa ufanisi mfano ‘ABInBEV Voyager Plant Optimisation (VPO), ambayo tunaitumia, imeonyesha mafanikio makubwa na kufanya viwanda vyetu kuwa kioo katika kufanikisha ajenda ya Serikali ya kuwa na Tanzania ya viwanda”. Alisema.
Pia alisema kuwa anaweza kufanya kazi zake vizuri kutokana na ushirikiano mzuri anaopata kutoka kwa wafanyakazi wenzake “TBL ni tanuru la kupika wataalamu na imeajiri watu wenye uwezo mkubwa katika fani zao hivyo nafanya kazi na wataalamu ambao wana upeo mkubwa na wanaoelewa nini wanachokifanya bila kuhitaji usimamizi mkubwa pia inatoa fursa kwa wafanyakazi wa jinsia zote kusimamia vitengo na mawazo yao kuheshimiwa.
Kuhusu changamoto anazokumbana nazo katika kazi yake alisema ni za kawaida na kutokana na elimu yake na uzoefu wa kazi alionao anaweza kuzitatua kwa urahisi na maisha kuendela kama kawaida.
Lina Ndemfoo,alisema kuwa anajivunia kufanya kazi na kampuni kubwa kama TBL ambayo imemuwezesha kujifunza mambo mengi ikiwemo kupata mafanikio mbalimbali katika maisha yake mojawapo ikiwa ni maendeleo yake binafsi.
Malengo yake ya baadaye ni kujiendeleza zaidi kielimu ili kwendana na mabadiliko ya kiteknolojia yanayotokea kila siku hususani katika kipindi hiki ambacho sekta ya viwanda inazidi kukua kwa kasi na kuhitaji wataalamu tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Anatoa wito kwa vijana wa kitanzania hasa Wasichana, kutokimbia masomo ya sayansi wanapokuwa mashuleni bali wajitahidi kukomaa nayo kwa kuwa katika dunia hii ya sayansi na teknolojia bila wataalamu katika nyanja hii itakuwa vigumu kwa taifa kupiga hatua ya maendeleo.