Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Zainab Chaula akifungua Mkutano wa Makatibu Wakuu wa Wizara ya Afya kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini Mwa Afrika (SADC), ambao ni moja ya vikao vya Mkutano wa Mawaziri wa Wizara hiyo kwa nchi za SADC, Mkutano huo unaendelea katika Ukumbi wa Mikutano Benki Kuu ya Tanzania Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Zainab Chaula, akiwa katika picha ya pamoja na Makatibu Wakuu na Wakuu wa Sekta ya Afya Kutoka Nchi 16 za Jumuiy ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) mara baada yakufungua Mkutano wa Afya na UKIMWI unaoendelea katika Ukumbi wa Mikutano Benki Kuu ya Tanzania Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Zainab Chaula, akiwa katika picha ya pamoja na Kamti ya Maandalizi ya Mkutano wa Mawaziri wa Afya na UKIMWI kwa nchi Wanachama wa SADC mara baada yakufungua Mkutano huo unaoendelea katika Ukumbi wa Mikutano Benki Kuu ya Tanzania Jijini Dar es Salaam.
Makatibu Wakuu na Wajumbe wa Sekta ya Afya kutoka nchi Wanachama SADC wakifuatilia ufunguzi wa Mkutano wa Afya na UKIMWI wa Mawaziri Wizara ya Afya unaoendelea katika Ukumbi wa Mikutano Benki Kuu ya Tanzania.
(Picha na Idara ya Habari-MAELEZO)
…………………..
Na. Paschal Dotto-MAELEZO.
Mkutano wa Mawaziri wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika SADC, Sekta ya Afya umeanza rasmi Jijini Dar es Salaam kwa Kutanguliwa na Kikao cha Makatabu Wakuu wa Wizara ya Afya kutoka nchi wanachama, huku ajenda 13 zikitajwa kujadiliwa katika Mkutano huo uonafanyika katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT).
Akizungumza katika Ufunguzi Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Dkt.Zainab Chaula amesema kuwa katika kati ya ajenda hizo 13, Kifua Kikuu itakuwa ni ajenda ambayo italengwa zaidi kwani malengo ya nchi za SADC ni kupunguza ugonjwa huo kwa kiasi kikubwa au kuufuta kabisa ifikapo 2030.
“Ajenda kubwa kati ya zile 13 katika Mkutano huu ni ile ya kupunguza ugonjwa wa kifua kikuu au kukomesha kabisa kwa nchi wanachama wa SADC, kwani malengo ya nchi hizi 16 ni kukomesha TB ifikapo mwaka 2030”, Alisema Dkt.Chaula.
Dkt.Chaula alisema kuwa ajenda nyingine ni pamoja na kupambana na maambukizi ya virusi vya ukimwi, masuala ya malaria, Afya ya mama na mtoto, chanjo ya mtoto, masuala ya lishe bora, utapiamlo na viribatumbo, uimarishwaji wa mfumo wa Afya hususani upatikanaji wa dawa na upatikanaji wa takwimu za Afya, rasilimali watu, rasilimali fedha na masuala ya ununuzi wa dawa ambapo Bohari Kuu ya Dawa kutoka Tanzania(MSD) inafanya kazi ya ununuzi na kusambaza dawa kwenye nchi za kusini mwa Afrika.
Ili kutekeleza azma hiyo, Mawaziri wa Sekta ya Afya kwa Nchi za SADC makatibu wakuu na wajumbe mbalimbali tayari wameanza kuandaa ajenda hizo, na mwitikio wa mahudhurio kwa wajumbe umekuwa mkubwa ambapo mpaka sasa ni asilimia 95.
Aidha Dkt. Chaula alisema kuwa, Tanzania imepewa heshima ya kuwa wanunuzi na wasambazaji wa dawa kwa nchi za SADC kwa hiyo Mawaziri watapata nafasi ya kutembelea Bohari Kuu ya dawa pamoja na kiwanda Kikubwa cha viua dudu cha kibaha.
“Mawaziri kutoka Nchi Wanachama wa SADC watapata fursa ya kutembelea kiwanda cha viua dudu Kibaha, kwa kuwa uwezo wake sasa umekuwa ni mkubwa na mnajua sasa hivi ajenda kama nchi ni kuhakikisha Tanzania inakuwa na uchumi wa kati wenye viwanda, kwa hiyo kiwanda hiki pia kinatuwakilisha kwenye nchi hizi za SADC”, alisema Dkt. Chaula.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dkt. Leonard Maboko amesema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kukabiliana na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI baada ya kufanikisha kwa kiasi kikubwa tohara kwa wanaume.
“Tunaingia na ajenda tulizowekeana katika kipindi kilichopita, sisi Tanzania kuna eneo ambalo tumefanya vizuri kuliko nchi zote za ukanda huu katika kupambana na maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI eneo hilo ni tohara kwa wanaume, kwa hiyo katika mkutano huu tutabadilishana uzoefu katika eneo la mafanikio kwa kila nchi kwa nchi 16 za SADC”, Alisema Dkt. Maboko.