Home Mchanganyiko KITUO CHA AFYA CHALINZE CHAKABILIWA NA UCHAKAVU WA BAADHI YA MAJENGO HUKU...

KITUO CHA AFYA CHALINZE CHAKABILIWA NA UCHAKAVU WA BAADHI YA MAJENGO HUKU KIKIHUDUMIA WAGONJWA TAKRIBAN 300 KWA SIKU

0
Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze
KITUO cha afya Chalinze, wilayani Bagamoyo, Pwani, kinakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa baadhi ya majengo ,upungufu wa majengo,watumishi,kukosa uzio,huku kikiwa kinahemewa kupokea wagonjwa  takriban 300 kwa siku. 
Kituo hicho kilianza kama zahanati mwaka 1982 kabla ya kupandishwa hadhi mwaka 1996 kuwa kituo cha afya, majengo yake  yamekuwa chakavu.
Mganga Mfawidhi wa kituo hicho Dkt. Sudi Msakamali, aliyasema hayo baada mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete na uongozi wa shule ya msingi Chalinze Modern Islamic kwenda kufanya usafi pamoja na kukabidhi msaada wa sabuni za maji na za unga kwa ajili ya usafi kituoni hapo.
Msakamali alisema , kituo hicho kinapokea wagonjwa 300 kwa siku, huku kikizalisha watoto kati 130 mpaka 150 kwa mwezi.
“Changamoto kubwa ni kuboreshwa miundombinu ya majengo, sababu wagonjwa wanaokuja kupatiwa matibabu ni wengi, idadi ya majengo ni ndogo hivyo kusababisha foleni na msongamano, na kutokuwepo uzio ,” alisema Dkt. Msakamali.
Akizungumzia changamoto hiyo, Ridhiwani aliipongeza shule ya msingi Chalinze Modern kwa namna wanavyojitoa katika kufanikisha maendeleo, ikiwemo kutoa msaada wa mifuko kumi ya saruji na karatasi nyeupe rimu 15 kwenye shule ya msingi ya Kibiki.
Alifafanua ,serikali imeshaanza kuzitafutia ufumbuzi changamoto ya uhaba wa watumishi,madawa na kwamba TACAIDS imeshaanza ujenzi wa  maabara itayojihusisha na upimaji wa vipimo vyote ikiwemo ya damu.
Akikabidhi sabuni za maji chupa 10, miche 15 ya sabuni ya kufulia na kiroba cha sabuni ya unga, Mkurugenzi wa shule ya msingi Chalinze Modern Omary Swed alibainisha shule yao imejitoa kwa ari na mali kushiriki kusaidia shughuli za kijamii.
“Shule yetu ya Chalinze imekuwa mstari wa mbele kusaidia shughuli za kimaendeleo katika nyanja tofauti, juzi tulikwenda shule ya msingi ya Kibiki tumesaidia mifuko kumi ya saruji na rimu 15 za karatasi kwa ajili ya mitihani,” alisema Swed.