Na Dotto Mwaibale, Dodoma
MKUU wa Wilaya ya Arumeru Jerry Muro anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Tamasha la muziki na fursa litakalo fanyika Mererani mkoani Arusha.
Akizunguza na waandishi wa habari jijini Dodoma juzi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMOFA) Stella Joel alisema tamasha hilo limeandaliwa na Tamofa na kuwa litafanyika Oktoba 28 hadi Novemba 3 mwaka huu.
” Tamasha ili litafanyika Oktoba 28 hadi Novemba 3, 2019 Viwanja vya Kanisa la International EAGT Mererani na litahudhuriwa na waimbaji wa muziki wa injili kutoka sehemu mbalimbali” alisema Stella.
Alisema lengo la tamasha hilo ni kwa ajili ya kuwapa fursa kwa wanamuziki wa mikoa ya Manyara na Arusha kuweza kuelewa faida zitokanazo na kazi zao pamoja na kuhakikisha wanasajili kazi zao Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA)
Joel aliwataja baadhi ya waimbaji wa nyimbo za injili watakao toa burudani katika tamasha hilo kuwa ni Mary Nyerere, Emmanuel Mbasha, Faraja Ntaboba, Evmagreth Sembuche, Stella Joel na Dkt.Tumaini Msowoya.
Stella aliongeza kuwa katika tamasha hilo kutakuwepo na madaktari ambao watakuwa wakitoa ushauri wa kitabibu na upimaji wa afya na kuwaomba wananchi wa mikoa hiyo kujitokeza kwa wingi kushiriki.