NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
SERIKALI imesema haitomvumilia mtu yeyote atakaethubutu kukwamisha ujenzi wa viwanda ,ikiwa ni pamoja na kuzalisha ama kuingiza bidhaa bandia zinazochafua taswira ya viwanda vya ndani ya nchi na sifa ya nchi kijumla.
Aidha imezielekeza mamlaka za ukaguzi na udhibiti wa ubora ikiwemo Shirika la viwango Tanzania(TBS )na NEMC kutoa huduma stahiki kwa wawekezaji pasipo urasimu.
Akifungua maonyesho ya mara ya pili ya viwanda kwa niaba ya makamu wa Rais ,katika viwanja vya ofisi ya mkuu wa mkoa wa Pwani, Naibu Waziri Wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji ,Stella Manyanya alisema haitowezekana kuwafumbia wale wachache wanaokwamisha juhudi za serikali za kukimbilia uchumi wa kati.
Alieleza ,serikali pia inaangalia utitiri wa kodi unaotozwa na tozo zinazotozwa na mamlaka za ukaguzi na udhibiti ubora unaolalamikiwa na wawekezaji.
“Hatua ya ushuru na tozo kuzifuta zimechukuliwa ,kati ya 114 zinazotozwa na taasisi za ukaguzi na udhibiti wa ubora wa bidhaa ,ambapo mwaka 2019 tozo 54 zimefutwa “
Stella alifafanua, licha ya viwanda kuzalisha bidhaa zenye viwango na ubora zinakumbana na ushindani sokoni.
Wakati huo huo ,alibainisha serikali inaendelea kuboresha reli na kujenga reli ya kisasa ili kusafirisha mizigo kwa kasi,kununua ndege kubwa kwaajili ya mizigo na kurahisisha sekta ya usafirishaji .
Pia Stella alisema, kuwekeza upatikanaji wa umeme wa uhakika vijijini na mijini na kuongeza ufanisi na utoaji mizigo bandarini.
Awali mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM ,mkoani Pwani Ramadhani Maneno alisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,ameonyesha dhamira ya kufufua sekta ya viwanda na kupigania kuinua sekta ya uwekezaji.
Alisema kauli ya mh.Rais imetekelezwa kwa vitendo mkoani Pwani na mkuu wa mkoa huo ameitendea haki utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Nae mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo alisema,kauli mbiu ya maonyesho hayo ni IJENGE TANZANIA,WEKEZA PWANI MAHALI SAHIHI KWA UWEKEZAJI .
Alisema, mkoa huo umevunja rekodi ya kuinua sekta ya uwekezaji na ujenzi wa viwanda zaidi ya 1,000 na kati ya hivyo 300 vimejengwa katika awamu ya tano na hii imetokana na kutokuwa na urasimu kwa wawekezaji na kutenga maeneo mengi kwa ajili ya viwanda.
“Malengo ya maonyesho haya ni kuonyesha kwamba mkoa umedhamiria kuwa ukanda wa viwanda,wenye viwanda kupata masoko ya uhakika,kupanua wigo wa soko la ndani ya mkoa kufikia kimataifa na ,kuvutia wawekezaji wapya”alisema Ndikilo.
Ndikilo alisema hali ya ushiriki imeimarika tofauti na mwaka jana ambapo mwaka huu wamefikia washiriki 329 na mwaka uliopita walikuwa 166.
Hata hivyo Ndikilo alibainisha, ,maonyesho hayo yataambatana na kongamano la uwekezaji litakalofanyika octoba 19 na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Wazir Mkuu Kassim Majaliwa.
Naibu Wazir wa Nishati,Subira Mgalu anatambua kuna maeneo yenye tatizo la kukatika umeme ila wanafanya kila linalowezekana kuwe na umeme wa uhakika.
Alisema tatizo hilo litakuwa historia baada ya kukamilisha miradi mikubwa ya Peri urban,ujazilizi ,stigo huko Rufiji wa megawatt 2,100 ili kupunguza tatizo la umeme maeneo ya vijijini na kwa wawekezaji.
Waratibu wa maonyesho hayo ni kampuni ya magazeti ya serikali (TSN) pamoja na mamlaka ya maendeleo ya viwanda (TANTRADE) .
Maonyesho hayo yanatarajia kufungwa octoba 23 mwaka huu na Waziri Mkuu Mstaafu ,Mizengo Pinda.