Baada ya ligi mbalimbali kuanza kutimua vumbi dunia nzima, kumekuwa na baadhi ya matokeo ya kushangaza kama ilivyo kila msimu.
Kwenye ligi kuu ya soka kule England (EPL) matokeo wanayoyapata Tottenham katika michezo minane ya kwanza yameshangaza wengi hasa kutokana na uwezo waliouonyesha msimu uliopita na hvy utabiri wa wachambuzi wengi ilikuwa na kuiona Tottenham msimu huu wakiuendeleza moto huo.
Hadi sasa ingawa ni mapema sana lakini Tottenham wamecheza michezo minane, wame poteza michezo mitatu, wamesare mara mbili na kushinda michezo mitatu pekee na kujikusanyia alama kumi na moja tu.
Kipigo kikubwa zaidi kwenye ligi ya mabingwa walichokipata katika mchezo wa kwanza tena nyumbani kwa kupigwa magoli 7 na Bayern Munichen, kilitibua hali ya hewa na kuchochea mgogoro wa chinichini kwenye klabu hiyo.
Msimu uliopita Tottenham walicheza fainali ya ligi ya mabingwa barani ulaya, ukawa ni msimu wa kukumbukwa katika historia ya klabu hiyo.
Ni wakati huu Tottenham wamefanikiwa pia kujenga uwanja wao mpya ambao una uwezo wa kuchukua mashabiki zaidi ya sitini elfu na kuuhama uwanja wao wa zamani.
Kwa mafanikio haya ya karibuni Tottenham wanaonekana kunogewa na wameanza kumjadili mwalimu aliyewapa mafanikio haya Mauricio Potchetino kama anatosha au lah!
Ni wazi kwamba matokeo yanapokuwa mabaya anaelaumiwa zaidi na kuwajibishwa ni kocha.
Lakini bado ukweli unabaki pale pale kwamba ili kocha afanye vizuri ni lazima kuwe na mazingira bora yatakayomwezesha kocha kuendelea kufanya vizuri.
Moja kati ya mazingira bora ni pamoja na ununuzi wa wachezaji bora watakaoweza kuipigania klabu.
Kwa misimu mitatu ya karibuni kikosi cha Tottenham hakina nyongeza ya wachezaji kwa maana ya kwamba hakuna ununuzi wa wachezaji uliofanyika.
Kwa sasa ili kuweza kushindania ubingwa ni lazima kufanya uwekezaji mkubwa hasa ununuzi wa wachezaji bora na kuwa na kikosi kipana kinachoshabihiana kwa ubora.
Pamoja na kufikiria kumfukuza Potchetino lakini pia ili kupata mafanikio wanayoyaota ambayo wameonja tamu yake, ni lazima kuhakikisha wanawekeza katika ununuzi wa wachezaji bora pamoja na kuboresha maslahi yao.
Tottenham wakumbuke tu kwamba ni vigumu sana kufaidi utamu wa tende bila kuuhudumia mtende wenyewe