**************************
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imetakiwa kuendelea kujihimiza zaidi
kusimamia mashauri yote yanayofunguliwa dhidi ya Serikali hatua
itakayoiwezesha Serikali kufikia malengo yake iliyojiwekea.
Hayo yamezungumzwa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,
Mhe.Prof. Ibrahim Hamis Juma alipomkaribisha Wakili Mkuu wa
Serikali na ujumbe wake ofisini kwake mapema leo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao hicho kilichokuwa na lengo la
kumtambulisha Naibu Mkuu wa Serikali Bwana. Gabriel Malata, Jaji
Mkuu Mhe. Prof. Juma ameitaka Ofisi ya wakili Mkuu wa Serikali
kuendelea kuboresha maeneo mbalimbali yenye mapungufu kwa lengo
la kuboresha huduma zake ili kuwafikia watu wengi zaidi kwa wakati.
Jaji Mkuu ameongeza kuwa utendaji wa Ofisi hiyo unatakiwa kuwa wa
hali ya juu sana kwa kuzingatia ukweli kuwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa
Serikali inayo wajibu mkubwa wa kusimamia mashauri yote
yanayoihusu Serikali kwa maslahi mapana ya taifa.
Prof. Juma ameongeza kuwa majukumu ya ofisi hiyo yanapaswa
kusimamiwa ipasavyo kwani umuhimu wake hujidhihirisha hasa pale
serikali inaposhitakiwa kwa mashauri makubwa ya kitaifa na kimataifa
kwani Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ndio inayobeba mzigo
kuhakikisha serikali inapata haki yake kwa wakati.
Aidha amewataka viongozi hao kufanya kazi kwa ukaribu ili waweze
kujenga mifumo madhubuti ya ufanyaji kazi ili waweze kuaminiwa na
jamii na kusisitiza kuwa jambo hilo litaifanya ofisi iendelee kujijengea
heshima kitaifa na kimataifa.
Katika hatua nyingine amewataka viongozi kuendelea kusimamia sheria,
taratibu na kanuni ili kuwasaidia mawakili wa serikali kuendelea
kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi kitaluma, maadili ya kazi na sheria, ikiwa ni pamoja na kujifunza zaidi, kuwa na hali na
molali ya kazi na kuhifadhi maarifa ikiwemo katika maktaba binafsi.
Amesisitiza kuwa isingefaa wakati zinapoitwa Mahakamani kesi zote
zinazohusu serikali, mawakili wa serikali wakawa hawajajiandaa, waoga
na wasiojiamini.
Alisema kuwa mawakili wa serikali wanapaswa kuwa waadilifu, wenye
kujituma wakati wote na kufuata maelekezo ya Mahakama pamoja na
kuyatafsiri vyema ili waweze kuyatumia kwa ufasaha katika kujenga
hoja zao.
Jaji Mkuu pia ameiasa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na ile ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa na utaratibu utakao wawezesha
kukutana mara kwa mara ili waweze kujadili na kuainisha changamoto
wanazokutananazo kwa ujumla ili kuhakikisha haki inatendeka kwa
wakati.
Kuhusu utekelezaji wa amri za Mahakama, Jaji Mkuu Mhe.Juma
amemuomba Wakili Mkuu wa Serikali kutumia mifumo mizuri ndani ya
serikali ili kuhakikisha kuwa maamuzi ya Mahakama yanatekelezwa ili
haki iweze kupatikana kwa wakati.
Akielezea uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika baadae
mwaka huu, kiongozi huyo ameitaka Ofisi hiyo kujikita zaidi katika
maandalizi ya kitaaluma ili pale zinapofunguliwa kesi za uchaguzi
kusiwepo na hoja zinazoweza kukwamisha uendeshaji wa mashauri
hayo.
Kwa upande wake Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Clement Mashamba
amemshukuru Jaji Mkuu kwa kumkalisha ofisini kwake huku akiahidi
kuufanyia kazi ushauri wake kwani mambo yote yaliyozungumzwa ni
changamoto zenye lengo la kutatua dosari zilizopo.
Ameendelea kueleza kuwa kama serikali wataendelea kutoa ushirikiano
unaohitajika kwa Mahakama ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wakati
hatua itakayosaidia serikali kutekeleza malengo yake kwa wakati.
Naye Wakili Mkuu wa Serikali Bwa. Gabriel Paschal Malata
amemshukuru Mheshimiwa Rais kwa kumteua katika nafasi hiyo na
kuahidi kuwa ataendelea kutimiza majukumu yake kwa ufasaha ili
kuhakikisha anamsaidia Mhe. Rais kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
“Namshukuru Mhe, Rais John Pombe Magufuli kwa kuniamini na
kunifanya kuwa miongoni mwa watu aliowaamini kuitumikia Ofisi ya
Wakili Mkuu wa Serikali,” alisema Bwa. Malata.
Aidha amemuahidi Jaji Mkuu Mhe. Prof. Juma kumpa ushirikiano na
kushughulikia changamoto zote ambazo zimekuwa kikwazo kwa Ofisi
ya Wakili Mkuu wa Serikali kutotekeleza majukumu yake kwa ufasa.
Wakati huo huo Naibu Wakili Mkuu amesema kuwa atahakikisha
anajenga mifumo imara itakayosaidia kuwajengea uwezo mawakili wa
serikali ili waweze kuiwakilisha vyema serikali katika mashauri
mbalimbali wawapo mahakamani huku akiuomba mhimili huo muhimu
wa serikali kuendelea kuipa ushirikiano Ofisi ya Wakili Mkuu wa
Serikali.
Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Msajili wa Mahakama Kuu ya
Tanzania Mhe. Katarina Revocati na wakurugenzi wa vitengo vya sheria
kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.
Wakuu wa vitengo walioambatana na viongozi hao ni Mkuu wa
mashauri ya Madai Bwa. Vincent Tangoh, Mkurugenzi wa Mashauri na
ubora Bwa. Evarist Mashiba na Mkurugenzi wa Usuluhishi Bwa. George
Mandepo.