Home Burudani Twanga Pepeta, Nguza, Papii kocha jukwaa moja Jumamosi

Twanga Pepeta, Nguza, Papii kocha jukwaa moja Jumamosi

0

********************************

Na Mwandishi wetu

Dar es Salaam.  Bendi ya muziki ya African Stars itafanya onyesho la pamoja na wanamuziki nyota nchini, Nguza Vikings na mwanaye, Papii Kocha kwenye ukumbi wa hotel ya Nefaland ya Magomeni Kagera.

Onyesho hilo limepangwa kufanyika Jumamosi ya Septemba 28  huku Nguza na Papii wakipania vilivyo kuonyesha makali yao kwa mara ya kwanza kwenye ukumbi huo.

Wakati Twanga Pepeta ambayo ipo chini ya ukurugenzi wa Luizer Mbutu inatarajia kutambulisha nyimbo kadhaa mpya, Nguza na Papii  kupitia bendi yao ya Big Sound wanatarajia kuweka hadharani vibao kadhaa vipya ambavyo wamevitunga hivi karibuni.

Mratibu wa onyesho hilo, Bakari Seif alisema kuwa onyesho hilo litaanza saa 2.00 jioni ili kutoa nafasi kwa mashabiki wa muziki wa dansi nchini kupata burudani inayoendana na kiingilio chao.

Alisema kuwa wanatarajia kupata shoo yenye ubora wa aina yake kwani Twanga Pepeta ni kisima cha burudani na Nguza na Papii ni moto wa kuotea mbali katika burudani.

“Hili ni onyesho maalum kwa mashabiki wa muziki wa dansi ambao wamekuwa wakimsubiri kwa hamu Twanga Pepeta na Nguza akiwa na Papii Kocha na bendi yake ya Big Sound. Nyimbo zote zinazotamba kwa bendi na wanamuziki hao zitapigwa ,.” alisema Seif.