Na Ramadhani Ali – Maelezo 25.9.2019
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka utaratibu wa muda wa uchimbaji wa kifusi, mawe, kokoto na matofali ya jasi kwa ajili ya miradi ya Serikali, wawekezaji na watu binafsi .
Akitoa tamko la Serikali kuhusu uratibu wa matumizi ya maliasili zisizorejesheka kupitia Shirika la Utangazaji Zanzibar, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalumu za SMZ Haji Omar Kheir amesema utaratibu huo unakusudia kuimarisha utekelezaji na utii wa sheria na uhifadhi wa mazingira.
Amesema Serikali imetoa ruhusa ya uchimbaji na usafirishaji wa maliasili zisizorejesheka kwa masharti maalumu yakiwemo kusajiliwa viwanda vyote vya kokoto kulingana na sheria Nam. 3 ya usimamizi wa mazingira ya 2015 na kuhakikisha kuwa wanauza kokoto kwa mtu mwenye stakbadhi ya malipo.
Ameyataja masharti mengine kuwa uchumbaji wowote wa Maliasili zisizorejesheka usizidi kina cha mita tatu kwenda chini, Miradi au wawekezaji wenye mahitaji ya kifusi, mawe au kokoto watalazimika kumuandikia Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi na kuainisha kiwango cha maliasili husika inayohitajika na sehemu atakayokwenda kuchukua.
Waziri Haji Omar Kheir ameyata maeneo yatakayotumika kwa uchimbaji mawe kwa Unguja kuwa ni Kibuteni, Zuze Dunga, Umbuji na Ndijani kwa Wilaya Kusini. Matemwe na, Kidoti Kaskazini Unguja na Wilaya ya Magharibi A ni Nyamanzi, Kisakasaka na maeneo mengine ya ukanda wa Magharibi.
Kwa Pemba ni muambe Wilaya ya Mkoani, Pujini na Vitongoji Wilaya ya Chake chake na Micheweni Wilaya ya Micheweni.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilisimamisha kwa muda uchimbaji wa kifusi, kokoto, mawe na matofali ya jasi ili kufanya tathmini na kuandaa mpango wa matumizi ya Maliasili zisizorejesheka tarehe 27.8.2019