Diwani wa Kata ya Mwangata katika manispaa ya Iringa Mhe.Nguvu Edward Chengula wapili kutoka kushoto akiwa katika ukaguzi wa miradi inayotekelezwa hivi karibuni
……………….
Na mwandishi wetu – Iringa
Diwani wa Kata ya Mwangata katika Manispaa ya Iringa, Mhe, Nguvu Edward Chengula kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi( CCM) amebainisha mpango wake wa kusukuma maendeleo ya Kata kwa kuwashirikisha wananchi na kutatua kero mbalimbali za Kata hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa Ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Kata hiyo, , Mhe, Chengula amebainisha maeneo mbalimbali anayoshiriki katika kuleta maendeleo ya Kata na wananchi kwa ujumla.
Kiongozi huyo ameyataja maeneo muhimu kuwa ni Umeme, Maji, Elimu na kilimo ambapo amekuwa akifanya kazi kwa kushirikiana na kamati za Shule kwa kuhakikisha shule zote zinaunganishiwa umeme sambamba na kupatiwa huduma ya maji.
“ Nawashukuru sana wananchi wa Kata ya Mwangata kwa ushirikiano wao kwani mara kwa mara wamekuwa mstaari wa mbele kujitoa na kushiriki moja kwa moja na mimi nimewaunga mkono hadi sasa shule zote za Msingi tayari zina umeme”. Amesema Diwani huyo.
Akiwa katika Shule ya msingi Kigamboni, kiongozi huyo ameeleza kuwa kwa sasa Shule hiyo inafanya kazi zake kwa urahisi baada ya kuunganishiwa umeme.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa shule ya Msingi Kigamboni Mwl. Grace Lyambilo ameeleza kuwa kwa sasa Shule ina maji na umeme na kubainisha kuwa wanafunzi wanapata uji kutokana na kuwepo kwa huduma ya maji.
“ Maji na umeme ni msaada mkubwa sana kwetu kiasi kwamba umeme umerahisisha kazi mbalimbali katika shule yetu ikiwa ni pamoja na suala la ulinzi”. Amebainisha Mwalimu huyo.
Miradi mingine inayo onekana kuchangia maendeleo ya Kata ya Mwangata ni pamoja na kuwapatia elimu wananchi juu ya Kilimo cha kisasa ambapo wananchi wanafundishwa kupitia mashamba darasa na mradi wa urasimishaji wa ardhi ambapo wananchi wanawezeshwa kupima viwanja vyao ili kupata hati miliki.