Ofisi ya Makamu wa Rais imefanya mapitio ya kanuni na kuandaa Kanuni mpya za Usimamizi wa Taka Hatarishi za mwaka 2019 kwa kuzingatia masharti ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira zilizotangazwa katika gazeti la Serikali na kupewa G.N 676 . Hayo yamesemwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Injinia Joseph Malongo alipokua akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam.
Altanabaisha kuwa kanuni hizo, zilionekana kuwa na mapungufu kadhaa hivyo kupelekea kuandaliwa kwa kanuni zingine. Mapungufu yaliyojitokeza ni kama vile Kifungu cha 133(1) na (3) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, kinampa mamlaka Waziri mwenye dhamana ya mazingira kutoa vibali vya kuingiza, kusafirisha nje ya nchi, kusafirisha ndani ya nchi au kupitisha taka hatarishi nchini. Hata hivyo Kanuni za mwaka 2009 zilitoa mamlaka hayo kwa Waziri na kwa Mkurugenzi wa Mazingira. Katika Kanuni mpya za mwaka 2019, mamlaka ya kutoa vibali yamebaki kwa Waziri mwenye dhamana ya mazingira tu akishauriwa na Mkurugenzi wa Mazingira.
Kanuni za mwaka 2009 hazikuweka bayana masharti ya kuzingatiwa na mmiliki wa kibali. Suala hili limezingatiwa katika Kanuni mpya za mwaka 2019. Uwepo wa masharti ya mmiliki wa kibali itarahisisha kufuatilia wa mwenendo wa uzingatiaji wa masharti yaliyoainishwa katika kibali cha usimamizi wa taka hatarishi pamoja na masuala ya hifadhi na usimamizi wa mazingira kwa ujumla wake.
Aidha alisema kuwa , kanuni za mwaka 2009 hazikuipa NEMC jukumu la kushughulikia maombi ya vibali kama sehemu ya mamlaka yake ya kusimamia uzingatiaji na utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira na Kanuni zake. Kanuni mpya za mwaka 2019 zimeandaliwa kwa kuzingatia Makundi ya aina za Taka Hatarishi kulingana na Mkataba wa Basel ambapo vyuma chakavu ni miongoni mwa taka zinazoweza kuwa hatarishi kwa kutegemea maeneo vinakochukuliwa au vinakohifadhiwa au jinsi vinavyosafirishwa hasa pale vinapochanganywa kutoka maeneo tofauti.
“Kanuni za mwaka 2019 zimeweka adhabu kali zaidi ukilinganisha na Kanuni za mwaka 2009 kwa makosa ya kutokuwa na kibali cha kusimamia taka hatarishi nchini. Adhabu hizo ni faini kuanzia milioni tano hadi bilioni kumi au kifungo kisichozidi miaka kumi na mbili au vyote kwa pamoja” alisema Injinia Malongo.
Ofisi ya Makamu wa Rais ina wajibu wa kusimamia Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira hapa nchini kwa mujibu kwa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 na Kanuni zake. Kanuni hizi pia zinapatikana katika Tovuti ya Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo ni www.vpo.go.tz na ile ya NEMC ambayo ni www.nemc.or.tz