UBORESHAJI wa miundombinu ya viwanja vya ndege na barabara kwa Nyanda za Juu Kusini kutachangia kukuza utalii kutokana na kuwa na vivutio vingi zaidi.
Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Akson alipozindua maonesho ya Karibu Utalii Kusini yanayofanyika kwenye Viwanja vya Kihesa-Kilolo, ambapo yanashirikisha taasisi za umma na watu binafsi.
Hatahivyo, Dkt. Akson amesema tayari amepata taarifa kuwa kuna matengenezo makubwa ya kiwanja cha ndege cha Iringa, ili kiweze kuhudumia ndege kubwa zaidi ya Bombardier ambayo inabeba abiria 72.
“Nimesikia hapa mkuu wa mkoa amesema kiwanja chetu cha hapa Iringa kitafanyiwa upanuzi mkubwa wa barabara ya kutua na kuruka ndege, na pia viwanja vya mikoa ya Mbeya, Mpanda, Songea na Katavi vyote vitaboreshwa zaidi,” amesema Dkt. Akson.
Lakini, amewataka wakazi wa Nyanda za Juu Kusini kuwa wabunifu kwa kuvutia watalii kutembelea vivutio vilivyopo, ikiwemo milima mingi, Hifadhi za Taifa za Ruaha, Mikumi, Udzungwa, Katavi na Kitulo; Kimondo cha Mbozi, Maporomoko ya Maji ya Kalambo na Ziwa Ngosi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli kwa kufanikisha upanuzi wa jengo la abiria na ukarabati wa barabara ya kutua na kuruka kwa ndege ya kiwanja hicho.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale amesema barabara ya kwenda kwenye Hifadhi ya Ruaha itaboreshwa, pamoja na Kiwanja cha ndege cha Iringa nacho kipo kwenye mchakato wa maboresho hayo.