Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Kisare Makori katika picha ya
pamoja na wajumbe kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na
wawakilishi kutoka China Academy of Building Research waliofika ofisini
kwake kwa ajili ya kupata taarifa zinazohusiana na utekelezaji wa mradi wa
ujenzi wa upanuzi wa JKCI wa awamu ya pili katika eneo la Mloganzila leo
Jijini Dar es Salaam. Mradi huo ni miongoni mwa matunda ya ziara ya Waziri
Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa aliyoifanya China mwaka 2018
Picha na: Genofeva Matemu – JKCI
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Kisare Makori akizungumza na
wajumbe kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) pamoja na
wawakilishi kutoka China Academy of Building Research waliofika ofisini
kwake kwa ajili ya kupata taarifa zinazohusiana na utekelezaji wa mradi wa
ujenzi wa upanuzi wa JKCI wa awamu ya pili katika eneo la Mloganzila leo
Jijini Dar es Salaam. Mradi huo ni miongoni mwa matunda ya ziara ya Waziri
Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa aliyoifanya China mwaka 2018
Baadhi ya wajumbe kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
pamoja na wawakilishi kutoka China Academy of Building Research
wakimsikiliza mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Kisare Makori (hayupo
pichani) wakati wa kikao kifupi kwa ajili ya kupata taarifa zinazohusiana na
utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa upanuzi wa JKCI wa awamu ya pili katika
eneo la Mloganzila leo Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wajumbe kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
pamoja na wawakilishi kutoka China Academy of Building Research
wakiangalia ramani ya eneo la Mloganzila wakati wa kikao kifupi kwa ajili ya
kupata taarifa zinazohusiana na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa upanuzi
wa JKCI wa awamu ya pili katika eneo la Mloganzila leo Jijini Dar es Salaam.
*********************
Na: Ales Mbilinyi – JKCI
11/09/2019 Serikali ya awamu ya tano kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) imejidhatiti kuboresha na kupanua miundombinu ya JKCI ili
kuifanya taasisi hiyo kuwa taasisi mahiri ya tiba ya magonjwa ya moyo kusini
mwa jangwa la sahara.
Akizungumza na waandishi wa habari walipotembelea Halmashauri ya
Ubungo kwa ajili ya kupata taarifa zinazohusu eneo litakapojengwa jengo
jipya kwa ajili ya upanuzi wa taasisi hiyo Afisa Mipango wa JKCI Vida Mushi
alisema kuwa kwa sasa taasisi inaufinyu wa eneo ukilinganisha na idadi ya
wagonjwa wanaopata matibabu katika taasisi hiyo.
“JKCI inaona wagonjwa kutoka nchi mbalimbali barani Afrika, ujenzi wa
upanuzi wa jengo jipya la JKCI katika eneo la Mloganzila umelenga kuifanya
JKCI kuwa taasisi mahiri ya tiba ya magonjwa ya moyo kusini mwa jangwa la
sahara” alisema Bi. Vida.
Aidha Bi. Vida alisema kuwa kwa sasa JKCI imewapokea wawakilishi kutoka
China Academy of Building Research waliokuja nchini kwa ajili ya kufanya
upembuzi yakinifu katika eneo la Mloganzila ikiwa ni maandalizi ya ujenzi wa
jengo jipya la Taasisi hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Kisare Makori
ameipongeza serikali kupitia JKCI kuhakikisha kuwa suala zima la matibabu
ya magonjwa ya moyo linapewa kipaumbele ukizingatia magonjwa ya moyo ni
magonjwa yanayokua kwa kasi.
“Serikali imekua ikitumia fedha nyingi kwa ajili ya matibabu ya watu wenye
magonjwa ya moyo nje ya nchi, huduma hizi kusogezwa karibu na wananchi
ni jambo la neema na itawasaidia wananchi wengi kutokulazimika kutumia
gharama nyingi kwenda kutibiwa magonjwa ya moyo nje ya nchi” alisema
Mhe. Makori.
Aidha Mhe. Makori alisema kuwa halmashauri ya Ubungo imewapokea
wataalamu kutoka China Academy of Building Research kwa ajili ya kupata
taarifa zinazohusiana na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa upanuzi wa JKCI wa awamu ya pili katika eneo la Mloganzila na kutoa ushirikiano kwa
kuwapatia taarifa zilizojitosheleza ili mradi huo uweze kukamilika kwa
wakati.
“Baadhi ya taarifa walizotaka kufahamu wakati wa upembuzi wa eneo la
mloganzila ni pamoja na miundombinu iliyopo katika eneo la mloganzila,
upatikanaji wa maji, upatikanaji wa umeme na vibali vyote vinavyohusika na
ujenzi, aidha tutaendelea kutoa ushirikiano katika hatua zote za ujenzi wa
mradi huo kwani ni mradi wa wamaendeleo kwa nchi yetu katika utoaji wa
huduma za afya” alisema Mhe. Makori