Home Mchanganyiko UMMY AWATAKIA HERI WATOTO WATAHINIWA DARASA LA SABA

UMMY AWATAKIA HERI WATOTO WATAHINIWA DARASA LA SABA

0

******************

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (Mb) amewapongeza na kuwatakia kila la kheri watoto wote wanaotarajia kuanza leo mtihani wa Taifa wa kuhitimu Elimu ya Msingi.

Waziri Ummy ameeleza kuwa, hatua waliyofikia watoto hawa ni fahari kubwa kwa wazazi, walezi na Taifa kwa ujumla kwani ni fursa adhimu kwa Ustawi na Maendeleo ya Mtoto na ni moja ya hatua ya kutimizwa kwa haki ya kumwendeleza na kumjengea mtoto msingi imara wa maisha yake ya baadae.

“Kipekee natoa pongezi zangu nyingi kwa watoto wote wa kike na wakiume walioweza kufikia hatua hii muhimu kwa maendeleo na ustawi wa watoto wa Kitanzania, ameeleza Mhe. Ummy”.

Taarifa ya Baraza la Mitihani zinaonyesha kuwa, jumla ya watoto 947,221 wavulana wakiwa 451,235 (sawa na asilimia 47.64), na wasichana 995,986 (sawa na asilimia 52.36) wamesajiliwa kufanya mtihani wa darasa la saba mwaka huu.

Ummy ameongeza kuwa, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya kupata elimu na kuendelea na masomo kuanzia elimu ya msingi hadi sekondari bila gharama zozote. Hivyo, amewataka kila mzazi na mlezi ametimize wajibu wake katika kuhakikisha kuwa watoto hawa wameandaliwa mazingira wenzeshi ya kutahiniwa na baadaye kuendelea na masomo ya sekondari, na vyuo vya ufundi vinavyotoa mafunzo katika stadi mbalimbali.

Aidha, imeelezwa kuwa jamii na wadau wanao wajibu wa kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kuwa watoto hawa wanendelezwa na wanalindwa dhidi ya vitendo vyote vya ukatili kwani bado ni watoto na wanayo haki ya kulindwa kwa mujibu wa sheria za Nchi.

Jamii imetakiwa ihusike kikamilifu kuimarisha ulinzi wa watoto wetu kwani ni kosa kutumia hila na kufanya mapenzi na mtoto, kufunga ndoa au kumhusisha Mtoto katika biashara au mahusiano yoyote yenye lengo la kingono iwe ni kwa malipo au bila malipo. Vitendo hivi havikubaliki.

Rai imetolewa kwa kila mwananchi kuendelea kufichua viovu kwa mamlaka za Serikali za Mitaa, Kijiji, Kata, Wilaya na hata katika Madawati ya jinsia na watoto yaliyopo kwenye vituo vya polisi nchini, mara wanapobaini dalili zozote za mzazi au mlezi au taasisi inaenda kinyume na jitihada za Serikali za kumwendeleza mtoto kielimu hasa katika kudhibiti ndoa kwa watoto waliomaliza elimu ya msingi. Mwisho, Waziri Ummy amewatakia mtihani mwema watoto wote mnaofanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba kwa mwaka 2019.