BARA la Afrika lina nafasi kubwa ya kupambana na umaskini na vikwazo vinavyozuia kuyafikia maendeleo na hiyo ni kutokana na kizazi cha sasa kuwa kizazi cha kwanza kabisa kuishi katika bara hilo wakishuhudia ukuaji wa uchumi ukifikia asilimia 4 kwa nchi nyingi barani humo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Afisa mtendaji mkuu wa taasisi ya The African Wildlife Kadu Sebunya amesema kuwa bara la Afrika tangu mwaka 1994 limeshuhudia vipindi virefu ya ukuaji wa kiuchumi tangu kipindi cha ukoloni katika miaka ya sitini, lakini bara la Afrika limeendelea kukua na kubadilisha fikra pamoja na kuyabadilisha mataifa mengi ya Afrika kwa kuwa na uchumi unaojitegemea na unaokua kwa kasi ulimwenguni.
Amesema kuwa uwekezaji katika tafiti, uvumbuzi, elimu, na huduma za afya umeendelea kupunguza kasi ya kuenea kwa magonjwa pamoja na kuongeza kasi ya kujiandikisha shule ambapo mamilioni ya watoto wanajiandikisha mashuleni kupata maarifa licha ya bara hilo kutokuwa katika nafasi nzuri katika masuala ya kisiasa.
Aidha amesema kuwa “Maendeleo ni Kuchagua” na hiyo itafanikiwa ikiwa viongozi wa Afrika na washirika wa maendeleo katika ngazi zote watapambana dhidi ya changamoto zinazozikumba nchi husika ikiwemo uchimbaji wa rasilimali, miundombinu hafifu, kilimo kisicho faafu, uharibifu wa mito, nyasi, mbuga za wanyama na misitu; vitu ambavyo wananchi wanavitegemea na hugharimu maendeleo.
Kadu amesema kuwa bara la Afrika ni mboni ya uhifadhi wa maliasili pamoja na viumbe wakiwemo robo tatu ya spishi za mamalia duniani wapatao 4700, ndege 2000,aina 2000 za samaki, na amfibia spishi 950 na hiyo ni pamoja na maelfu ya mimea yenye thamani pamoja na wanyama wa mwituni ambao wanawakilisha uasilia, uchumi na ikolojia.
Utajiri wa Bara hilo umeelezwa zaidi hasa katika sekta za mafuta na gesi asilia na hiyo ni pamoja na kuwa na kampuni zenye umiliki wa hifadhi ya madini wa asilimia 40 duniani licha ya mlengo wa majadiliano ya sasa kuhusiana na maendeleo Afrika yameegemea zaidi katika unyonyanyi wa rasilimali na namna bora ya kuyafikia maendeleo.
Imeelezwa kuwa bara la Afrika ina maelfu ya utajiri katika sekta za utalii, madini na gesi na kwa sasa kinachotakiwa ni kuangaza macho katika mambo ya msingi ikiwemo madini, miundombinu, mafuta na gesi asilia, kilimo, makazi na mifumo ya wanyama kutegemeana pamoja na usimamizi endelevu wa rasilimali zake asili za kiafrika, mazingira, wanyama pori pamoja na ardhi.
Kupitia mkutano huo Kadu amewashukuru watoa mada wa mkutano huo akiwemo Rais mstaafu wa awamu ya tatu Rais Benjamin Willium Mkapa na Rais Mogae kwa kushirikiana na taasisi hiyo katika msingi wa wanyamapori wa kiafrika na katika mada zao wamesisitiza mambo muhimu sana kuhusiana mazingira, wanyamapori, na maeneo ya porini na kueleza kufikia mwaka 2063 Afrika litakua bara la maendeleo lenye kutumia rasilimali zake kukiletea maendeleo na kuyasimamia.