Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Songwe Eliniko Mkola (aliyesimama) akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Songwe wakati wa kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha Januari Mpaka Juni 2019.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemus Mwangela akiwasilisha taarifa ya ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha Januari Mpaka Juni 2019 katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Songwe ambapo taarifa hiyo ilipokelewa na kupitishwa.
………………….
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Songwe Eliniko Mkola amewapiga marufuku viongozi wa Chama hicho Mkoani Songwe kutoa vitisho vya aina yoyote kwa Watumishi wa Serikali Mkoani hapa.
Mkola ametoa marufuku hiyo jana wakati wa kikao cha Halmashauri kuu ya CCM Mkoa wa Songwe kilichoketi kupotea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha Januari mpaka Juni 2019 ambapo taarifa hiyo ilipokelewa na kupitishwa.
“Liko tatizo la baadhi ya viongozi wa chama kusikiliza maneno na kutoyafanyia uchunguzi pia Wapo baadhi ya viongozi wa Chama hutishia viongozi wa Serikali, ni marufuku kwa vitendo hivyo kuanzia leo” amesisitiza Mkola.
Ameongeza kuwa taasisi zote zinafanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu hivyo ni vema kujenga mazoea ya kuzisoma ili viongozi wa chama na wale wa serikai kila mmoja ajue mipaka yake ya utendaji kazi.
Mkola ametoa rai kwa viongozi wa chama na serikali kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuujenga Mkoa wa Songwe kwani wote wana nia moja ya kuhakikisha maendeleo yanapatikana Mkoani hapa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemus Mwangela amesema viongozi wa serikali waliopo hawana nia ya kuuharibu Mkoa wa Songwe hivyo viongozi wa chama wawatumie katika kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo.
Brig. Jen. Mwangela ameongeza kuwa endapo viongozi wa chama wataona kuna mambo kwenye Mkoa au Halmashauri zao hayaendi vizuri wawasilishe masuala hayo kwa viongozi walioko Mkoani hapa ili yafanyiwe kazi na pia wajitahidi kuepuka misuguano isiyo ya lazima.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Songwe David Kafulila amesema Viongozi wa chama na Serikali wasioneane aibu kuelezana ukweli kuhusu mapungufu ya baadhi ya watendaji wa serikali kwani kufanya hivyo maendeleo ya Mkoa yatachelewa.