waandamanaji walioandamana katika Ubalozi wa Afrika ya Kusini
kushinikiza kuachiwa kwa ndege ya Shirika la ATCL inayoshikiliwa Jijiji Johanesberg nchini Afrika ya Kusini.
*****************
Na.Mwandishi Maalum –Dar es Salaam.
Katika hali isiyo ya kawaida mamia ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wameandamana kuelekea katika Ubalozi wa Afrika ya Kusini nchini kushinikiza kuachiwa kwa ndege ya ATCL inayoshikiliwa Jijini Johanesberg Afrika ya Kusini kwa amri ya Mahakama.
Maandamano hayo ambayo hayakufahamika yametokea upande gani wa Jiji yaliwashirikisha watu mbalimbali wakiwemo waliojitambulisha kama wanafunzi wa vyuo vya elimu ya Juu pamoja na wananchi wa kawaida waliodai wamechoshwa na vitendo vya kuihujumu serikali ya awamu ya Tano.
Mabango mbalimbali waliyobeba waaandamanaji hao yalionyesha kusikitishwa na kitendo cha kushikiliwa kwa ndege ya Tanzania nchini Afrika ya Kusini , nchi ambayo uhuru wake umepatikana kwa msaaada wa Tanzania kwa kuwasaidia makazi na hata vifaa waliokua wapigania uhuru wa nchi hiyo.
Mmoja wa waandamanaji hao ambaye hakutaka kutaja majina yake , akiongea kwa uchungu alisema Afrika ya Kusini imekua nchi isiyo na shukrani kabisa kwa kitendo cha kuikamata ndege ya ATCL ambalo ndilo kwanza linatoka katika hali ya kuwa taabani.
“Tumekuja hapa kuwaambia wenzetu wa Afrika ya Kusini kwamba uungwana sio tu kulipa fadhila kwa aliyekusaidia, bali hata matendo tu yanatosha, haiwezekani sisi tumewasaidia wapate uhuru leo hii hawana hata aibu wanakamata ndege yetu tena kwa sababu zisizokua na msingi” Alisema mmoja wa waandamanaji hao.
Mingoni mwa mabango waliyobeba yalisomeka ‘Turudishieni ndege yetu na sisi tuwarudishie makaburu uhuru wao maana mmeshindwa kuwa wasataarabu’ lingine lilisomeka ‘ Waafrika ndio maana tunadharaulika duniani kwa kufanya mambo ya hovyo.
Kwa upande wake Sadik Ramadhan aliyekua anazungumza kwa jazba alisema waafrika ya kusini ni rafiki zetu kitendo cha kushirikiana na mzungu mmoja kuihujumu Tanzania ni kitendo ambacho hakikubaliki kabisa, alisema Rais Ramaphosa alipokuwa nchini kwenye mkutano wa SADC aliwahakikishia watanzania kwamba undugu wa nchi hizi utaendelea na hakuna hata mtu mmoja wa kuuvunja.
Aidha alisema lengo la maandamano hayo ya amani ni kumtaka Balozi atoke na aeleze ni hatua gani zinazoendelea za kuhakikisha ndege ya watanzania inarudi kwani imenunuliwa kwa kodi za wananchi tena wananchi masikini wanaopambana kuinua nchi yao.
Huku wakiimba wimbo kwamba wamemsaliti mzee Mandela waandamanaji hao walisema inatia uchungu sana kuona taifa lililosaidiwa na Tanzania ndio sasa linakua mstari wa mbele kuhujumu mali zake jambo ambalo wamesema halikubaliki.
Maandamano hayo ambayo yalizua taharuki kwa takriban nusu saa, yalizimwa na Jeshi la polisi kwa kuwataka waandamanaji hao kuondoka kwa madai suala hilo linaendelea kushughulikiwa kwa mujibu wa sharia na taratibu za kidiplomasia.
Baada ya kuamriwa kuondoka waandamanaji walitawanyika wakiendelea kuimba kwamba ujume umefika na kilichobaki wanasubiria ndege yao na kama haitaachiwa watafanya ubalozi huo ushindwe kutekeleza kazi zake za kila siku kwani wataandamana mpaka kieleweke.
Kwa upande wake kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa alipofika kwenye ubalozi huo aliwataka waandamanaji kufuata sharia na kutojichukulia sharia mkononi kwani wanaweza kushitakiwa, aidha Jeshi la Polisi liliwatia nguvuni baadhi ya waandamanaji hao.
Hadi maandamano hayo yanavunjwa hakuna kiongozi yeyote wa ubalozi huo aliyejitokeza kusikiliza hoja za waandamanaji bali walijifungia ndani huku baadhi ya wafanyakazi wakionekana kuchungulia madirishani kuona nini kinaendelea , na wengine wakipiga picha kwa kutumia simu zao za kiganjani.