Na Estom Sanga -TASAF
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika, Bi.Anne Kabagambe amepongeza mafanikio ya Serikali ya Tanzania Kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF katika kuboresha maisha ya Wananchi wanaokabiliwa na Umaskini.
Bi. Kabagambe ambaye yuko nchini kwa ziara ya Kikazi , ametoa pongezi hizo baada ya kukutana na Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na TASAF,na kujionea bidhaa wanazozalisha katika Mtaa wa Keko Machungwa ,Wilaya Temeke, mkoani Dar es salaam.
Amesema kutokana na ubora wa Utekelezaji wa Miradi ya TASAF, Benki ya Dunia imekubaliana na Serikali ya Tanzania kuidhinisha kiasi cha Shilingi Trilioni Moja kwa ajili ya Utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Sehemu ya Pili , fedha ambazo amesema zitasaidia zaidi juhudi za Serikali katika kuwahudumia Wananchi wanaokabiliwa na Umaskini.
‘’Tumejiridhisha pasi na mashaka kuwa utekelezaji wa Shughuli za TASAF katika awamu zote tatu umekuwa wa mafanikio makubwa hivyo Benki ya Dunia imeamua kuendelea kusaidia juhudi hizi’’ amesisitiza Bi.Kabagambe.
Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika amesema kiasi hicho cha fedha kitatolewa mwezi Ujao wa Septemba na kuwataka Walengwa na Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kuendelea kuboresha miradi ya kiuchumi ili kuongeza tija na hatimaye waweze kuboresha zaidi maisha na kuondokana na umaskini wa kipato.
Kwa Upande wao Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wameishukuru Serikali kupitia TASAF kwa jitihada za kuwaondolea kero ya umaskini wa kipato na kuomba juhudi zaidi zielekezwe katika kuwapatia elimu ya Ujasiliamali ili waweze kuboresha shughuli za uzalishaji mali na kukuza kipato chao.
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii – TASAF umekuwa ukitekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambao unahudumia takribani Kaya Milioni Moja na Laki Moja Kote Tanzania Bara,Unguja na Pemba na hivi sasa uko katika maandalizi ya utekelezaji wa Sehemu ya Pili ya Mpango inayotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni baada ya taratibu muhimu kukamilika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika, Bi. Anne Kabagambe (aliyeshika mkoba) akilakiwa na Mmoja waMaafisa wa TASAF, Bi. Tatu Mwaruka wakati wa ziara ya kukutana na Walengwa wa TASAF katika Mtaa wa Keko Machungwa wilaya ya Temeke Jijini Dar es salaam.
Bi. Anne Kabagambe (picha ya juu na chini) akiwa katika mkutano na walengwa wa TASAF katika mtaa wa Keko Machungwa ,wilaya ya Temeke, jijini Dar es salaam.
Baadhi ya Walengwa wa TASAF wakiwa na bidhaa walizozitengeneza baada ya kupata ruzuku kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini-PSSN.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika Bi. Anne Kabagambe akikagua bidhaa zilizotengenezwa na Walengwa wa TASAF mtaa wa Keko Machungwa,Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya DuniaBi. Anne Kabagambe katika picha na Walengwa wa TASAF baada ya kukagua bidhaa wanazozitengeneza kama njia mojawapo ya kujiongezea kipato kkupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.