Home Mchanganyiko TCRS KUJA NA MTAALA WA KUWAFUNDISHA BIASHARA WAMACHINGA

TCRS KUJA NA MTAALA WA KUWAFUNDISHA BIASHARA WAMACHINGA

0

Meneja wa TCRS Mkoa wa Morogoro, Rehema Samweli, akizungumza wakati wa semina ya kujadili kuhusu kuanzishwa kwa mataala wa wafanya biashara ndogo ndogo. Picha na Victor Makinda

…………………………………………….

NA VICTOR  MAKINDA: MOROGORO

 

Taasisi isiyo ya kiserikali iyoshughulika na masuala ya wakimbizi ya Tanzania, TCRS, ipo mbioni kuja na mtaala wa elimu kwa ajili ya kuwafundisha mbinu sahihi za biashara,  wafanya biashara ndogo ndogo maaraufu kama machinga.

 

 Akizungumza wakati wa semina ya kujadili uanzishwaji wa mitaala kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo ndogo, iliyofanyika juzi mjini Morogoro, Meneja wa TCRS mkoa wa Morogoro, Rehema Samweli, alisema kuwa wao kama taasisi wamefanya tafiti na kubaini mapungufu mengi sambamba na changamoto nyingi zinazo kabili kundi la wafanya biashara ndogo ndogo.

 

“ Tumefanya utafiti mara tatu katika mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam na Dodoma na tumebaini changamoto nyingi zinazo wakabili wafanya biashara ndogo  ndogo na hivyo kwa sasa tunakusanya maoni ya wadau mbali mbali ili tuje na mtaala maalumu kuwafundisha wafanya biashara ndogo ndogo mbinu  bora za biashara ili waweze kujikwamua wao wenyewe na kuchangia katika pato la Taifa. Alisema Rehema.

 

Akitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili wafanya biashara ndogo ndogo ambazo wamezibaini katika utafiti wao walioufanya kwa  ufadhiri wa shirika la TCRS, Dkt Wambuka Rangi, Mtafiti kutoka Chuo Kikuu Huria Tanzania, alisema kuwa changamoto kwa wafanya biashara ndogo ndogo ni  kutokuwa na elimu ya kuweka kumbukumbu za biashara zao, ikiwa ni pamoja na kujua kiasi gani kimetumika kununua bidhaa na biadhaa hiyo iuzwe shilingi ngapi ikiwa na mchanganuo wa faida au  hasara.

 

“ Wafanya biashara ndogo ndogo, katika utafiti tulioufanya tumebaini kuwa wengi wao hawajui ni namna gani watapata mikopo ya riba nafuu na hivyo hukopa mikopo yenye riba kubwa ambayo haina tija kwao.  Tumebaini kuwa wengi wao hawajui masuala ya afya na usafi wao na mazingira, hawajui sheria ndogo ndogo za miji na majiji, ,hawafanyi utafiti wa kubaini soko gani linahitaji bidhaa gani, hawatumii lugha nzuri ya kumvutia mteja lakini pia tumebaini kuwa hawana nidhamu ya fedha sambamba na elimu ya kujitambua na kujikubali.” Alisema Dkt Wambuka.

 

 Haya na mengine mengi ndiyo masuala hasa yanayotupelekea kuja na mtaala maalumu wa kuwafundisha wafanya biashara ndogo ndogo ili waweze kuwa na elimu na maarifa ya  kufanya biashara kwa tija ili waboreshe maisha yao na jamii yao kwa ujumla.

 

 Kwa upande wake mshiriki wa semina hiyo,  Chuwa Haruni, ambaye ni mwenyekiti wa kikundi cha wafanyabiashara ndogondogo cha Umoja Group cha mjini Morogoro, alilipongeza wazo hilo la TCRS kuja na mitaala kwa ajili ya kuwafundisha wafanya biashara hizo huku akisema mtaala huo utakuwa ni mkombozi mkubwa kwao.

“ Ni kweli sisi wafanya biashara ndogo ndogo hatuna elimu yoyote ya biashara. Tunafanya biashara pasipo elimu wala ujuzi. Tunahitaji sana elimu juu ya nmna sahihi ya kufanya bisahara ambayo itatupa mwongozo wa kufanya biashara zetu kwa tija.” Alisema Chuwa.

 Naye Haji Sajilo Mfanyabisahara ndogo ndogo wa Manispaa ya Morogoro alisema kuwa  elimu ya biashara ni muhimu mno kwa wafanya biashara ndogo ndogo kwani wengi wao wanakabiliwa na tautizo la kutotunza kumbukumbu na hivyo wanafanya bishara kwa mazoea huku wakiwa hawajui ipi faida na ipi hasara na mwisho wake kuishia kufilisika,

 

 “ Mtaala huo ni mzuri sana. Ninaomba uje haraka, tena haraka sana. Ni elimu ambayo itatutoa hapa tulipo na kutupeleka hatua nyingine. Mali bila daftari hupotea. Tukifundishwa  njia sahihi ya namna ya kutunza kumbukumbu itatujengea uwezo wa kufanya biashara kwa faida na kuzalisha faida. Kwa sasa tunahangaika tu huku tukiwa hatuna mbinu, maarifa na elimu ya biashara ndio sababu unaweza kuona wafanya biashara ndogo ndogo 50 wote wanauza Radio. Ni kwa ajili ya kukosa mbinu na ubunifu hivyo hata biashara zetu ni za kuigana.

 

Afisa tawala msaidizi Wilaya ya Morogoro, Yahya Mohamed,  akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya katika semina hiyo, alisema kuwa mtaala huo utawapunguzia kazi wao viongozi kwa kuwa utakuwa umewapa mwanga mkubwa wafanya biashara ndogo ndogo kujua sheria za miji na majiji na hivyo kuwaondolea kazi ya kukimbizana nao kila uchao kwa kuwa wafanya bishara ndogo ndogo wamekuwa ni wakaidi wa sheria.

 

“Itatusaidia sana sisi kama Wilaya kwa kuwa tutakuwa na wafanya bisahara  watakao kuwa na uwelewa wa sheria na taratibu. Lakini pia hii itawaondolea hasara wanazozipata mara kwa mara kwa kutojua namna ya kutunza kumbukumbu na elimu juu ya mikopo. Wazo lenu TCRS ni zuri na sisi kama serikali tunalipongeza na tunaomba mlitekeleze kwa kuwa tija yake ni tija ya Taifa kwa ujumla.” Alisema Yahya.