Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu (kushoto) akiwa na mwenyeji wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TIB, Bw. Charles Singili (kulia) alipofanya ziara katika Benki hiyo jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19 katika taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango ili kujua changamoto na njia za kuzitatua kwa mwaka wa fedha 2019/20.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TIB, Bw. Charles Singili (kulia), akieleza kuhusu utoaji mikopo ya mitaji katika miradi ya Serikali na watu binafsi, wakati wa Mkutano na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu (kushoto), katika Ofisi za Benki hiyo jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu (kushoto), akiangalia machapisho ya Benki ya TIB na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Bw. Charles Singili akitoa maelezo, wakati wa ziara ya Naibu Katibu Mkuu huyo iliyolenga katika utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19 kwa taasisi hiyo ili kujua changamoto na njia za kuzitatua kwa mwaka wa fedha 2019/20.
Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Christopher Nkupama (kulia) na Mtaalam wa Mipango kutoka Wizara hiyo, Bw. Msabaha Msabaha, wakifuatilia mkutano kati ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Khatibu Kazungu na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TIB, Bw. Charles Singili (hawapo pichani), jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TIB, Bw. Charles Singili (kulia) akimuongoza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu (kushoto) kuangalia baadhi ya viongozi wa Benki hiyo kwa nyakati tofauti wakati wa ziara ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19 katika taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango ili kujua changamoto na njia za kuzitatua kwa mwaka wa fedha 2019/20.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu (katikati), akisalimiana na mmoja wa wateja wa Benki ya TIB, wakati wa ziara ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19 katika taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango ili kujua changamoto na njia za kuzitatua kwa mwaka wa fedha 2019/20, kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TIB, Bw. Charles Singili.
(Picha na Peter Haule, WFM, Dar es Salaam)
*************
Na. Peter Haule, WFM, Dar es Salaam
Serikali imeitaka Benki ya TIB kuhakikisha inawafuatilia kwa karibu wadaiwa sugu wote wa Benki hiyo ili waweze kurejesha fedha wanazodaiwa ili kuongeza ukwasi wa taasisi.
Hayo yameelezwa jijiji Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu, alipofanya ziara katika Benki hiyo ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19 katika taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango ili kujua changamoto na njia za kuzitatua kwa mwaka wa fedha 2019/20.
Dkt. Kazungu amesema, wadaiwa sugu wanaodaiwa na Benki ya TIB warejeshe fedha walizochukua ili kuongeza ukwasi wa Benki hiyo na kuendelea kukidhi vigezo vya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inavyoviangalia katika kudhibiti taasisi za kibenki nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TIB, Bw. Charles Singili, alisema kuwa ni vizuri watu wazingatie mikataba wanayoingia na Benki wakati wa kukopa fedha, kwa kujenga nidhamu ya matumizi ili kuzitumia katika lengo husika na kukuza uchumi wa mlengwa hatimaye kuzirudisha kwa wakati ili kutoa fursa kwa wengine kunufaika na mikopo hiyo.
“Benki ya TIB ni taasisi ya Serikali na ni ya kisera, imeundwa mahususi kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya uwekezaji wa ndani ya nchi hususani katika kufanikisha utekelezaji wa miradi ya Serikali na miradi ya sekta binafsi”, alieleza Bw. Singili.
Bw. Singili alisema kuwa, Benki ya TIB ilianzishwa ili kukabiliana na uhitaji wa mitaji ya muda mrefu kwa kuwa benki nyingi nchini ni za kibiashara na mitaji inayotoa kwa wateja wake ni ya muda mfupi.
Alisema kuwa mikopo inayotolewa na benki hiyo inaendana na ajenda ya Serikali ya kuboresha miundombinu wezeshi pamoja na uwekezaji kwenye viwanda, hivyo ajenda hiyo haiwezi kufikiwa kwa mikopo ya mitaji ya muda mfupi.
“Ukitazama Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka mitano 2016/17 hadi 2020/21 kwa fedha iliyopangwa kwa ajili ya kutekeleza mpango huo haiwezi kupatikana kutokana na makusanyo ya kodi pekee hivyo kuna kila sababu kwa taasisi hii kama Benki ya Maendeleo kuangalia njia mbadala hususani kupitia kwenye masoko ya mitaji ili kusaidia juhudi za Serikali katika upatikanaji wa fedha hizo”, aliongeza Bw. Singili.
Bw. Singili ameahidi kuyafanyia kazi maagizo ya Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Kazungu, hususani katika kukabiliana na mikopo chechefu kwa kuongeza nguvu katika kuwafuatilia wadaiwa sugu.
Aidha amempongeza Naibu Katibu Mkuu huyo, kwa kufanya ziara za kiutendaji katika taasisi yake, kwa kuwa zinasaidia katika kubadilishana mawazo na kujua matarajio na changamoto za taasisi katika mtazamo wa pamoja wa kuzitatua.