Home Uncategorized WATAFITI AKIOLOJIA WANAKABILIWA NA UKOSEFU WA VIFAA

WATAFITI AKIOLOJIA WANAKABILIWA NA UKOSEFU WA VIFAA

0

Mkuu wa wilaya ya Iringa, Asia Abdalah akizungumza wakati wa maadhimisho ya Miaka 128 tangu ushindi wa chifu Mkwawa dhidi ya askari wa kijerumani.

Mkuu wa wilaya ya Iringa, Asia Abdalah akifanya utafiti wa kuangalia masalia ya Vita Kati ya askari wa chifu Mkwawa na askari wa kijerumani. 

****************

NA DENIS MLOWE, IRINGA

WANAFUNZI wanaofanya mafunzo kwa vitendo kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam Idara ya Akiolojia juu ya utafiti wa masuala ya kihistoria wanakabilwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa vifaa.

Akizungumza wakati wa kuadhimisha miaka 128 tangu ushindi wa Chifu Mkwawa dhidi ya askari wa Kijerumani na kufanyika katika eneo lilipojengwa mnara wa kumbukumbu eneo la Lugalo katika wilaya ya Kilolo,Mwanafunzi wa Mwaka wa pili chuoni hapo, Amani Kalwani alisema kuwa changamoto hizo zinatokana na kutokuwepo kwa vifaa vya kufanyia utafiti.

Alisema kuwa utafiti wanaofanya ni kuhusu masalia ya vita lengo kubaini vitu vilivyotumika katika mapigano na njia zilizotumika katika vita hiyo baina ya askari wa chifu Mkwawa na askari wa Kijerumani ambapo walipigana vita eneo la Lugalo na kukutana na changamoto zikiwemo ukosefu wa vifaa vya uchunguzi.

Alisema kuwa changamoto nyingine ni ukosefu wa huduma za jamii zikiwemo maji safi na salama, umeme, huduma za afya ambapo wanafata zaidi ya km 25 Iringa mjini hali ambayo inafanya suala la utafiti kuwa mgumu zaidi.

Kalwani alisema kuwa changamoto nyingine wanayokumbana nayo katika utafiti huo ni suala zima la posho ya kujikimu hali inayowakabili wanafunzi wengi walioko katika utafiti huo na kutoa wito kwa bodi ya mikopo kutoa posho linganifu kwa wanafunzi wote.

Alisema kuwa kuna haja kubwa ya bodi ya mikopo kuangalia kwa umakini suala ya posho ya kujikimu kwani wanafunzi wengine wanapata hela kidogo hali inayofanya asilimia kubwa kufanya utafiti kwa kujitolea licha ya utafiti huo kuwa faida kwa taifa hasa katika masuala ya historia.

“Kutambua mafunzo na mchango wa utafiti ipo haja ya bodi ya mikopo iweke ulinganifu wa posho za kujikimu kama ilivyo katika kada ya ualimu hali itakayosaidia wanafunzi wengi kufanya vyema katika utafiti wanaofanya” alisema

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kitivo cha Akiolojia, Dk Frank Masele, alisema kuwa utafiti wa mwaka jana ulifanyika bila kuwa na vifaa vya kisasa hali iliyomlazimu utafiti wa mwaka huu kutumia fedha za kujikimu kupata mashine moja ya kufanyia utafiti kwa lengo la kubaini mabaki yaliyotumika katika vita kati ya Askari wa chifu Mkwawa na askari wa kijerumani.

Alisema kuwa utafiti huo unafanyika katika mazingira magumu kwa wanafunzi na kulazimika kuishi katika nyumba moja kwa kuchangishana ili kuweza kuwapatia mafunzo kwa vitendo juu ya kuitambua historia ya nchi katika harakati za ukombozi.

Dk. Masela alisema kuwa maadhimisho hayo yanatumika kutoa elimu kwa jamii inayozunguka kutambua juu ya historia za mashujaa na utafiti huo utafanyika kwa miaka 3 ingawa changamoto kubwa ya wanafunzi wanayopata ni ukosefu wa fedha.

Alisema kuwa kuwe na fungu la kutosha la kuwawezesha wanafunzi kuweza kufanya utafiti kwani kuna mazingira magumu ya ufundishaji hasa somo la Akiolojia ambalo asilimia kubwa mazingira yake makubwa ni porini ambapo wanakumbana na vitu hatarishi mbalimbali ikiwemo nyoka wenye sumu kali;.

Alisema kuwa katika utafiti wanaofanya kwa mwaka jana ambao walikuwa hawana vifaa walifanikiwa kupata masalia 14 ya maganda ya risasi yaliyotumika katika vita na mwaka huu kwa wiki mbili wamefanikiwa kupata masalia 6 hali ambayo wanatarajia kupata vitu vingi zaidi.

Alisema kuwa utafiti wanaofanya mwaka huu wanatarajia kuangalia njia mbalimbali zilizotumika katika vita baina ya Askari wa Chifu Mkwawa na Askari wa Kijerumani na ukubwa wa eneo la vita ambalo walitumia kupigana mwaka  na Mkwawa kupata ushindi mwaka 1891.

Naye mkuu wa wilaya ya Iringa, Asia Abdalah alisema kuwa ifike wakati sehemu zote zenye vivutio ziweze kuleta faida kwa serikali wa watalii kutembelea na kuleta mapato. 

Alisema eneo la Lugalo muhimu kuzungushiwa uzio ili ifike wakati watu waweze kulipa kiingilio na kuleta mapato kwa wilaya na taifa kwa ujumla kuliko ilivyo sasa.