LORI jingine la mafuta aina ya Scania, lenye namba ya usajili T 243 BCU, na tela T 685 DCV mali ya kampuni ya Njombe Filling Station, limeteketea kwa moto baada ya kupata ajali katika Kijiji cha Ngadinda Halmashauri ya Madaba, Ruvuma.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma (RPC), Simon Maigwa Marwa, amethibitisha tukio hilo.
“Tukio la ajali ni kweli limetokea jana saa nne usiku (kuamkia leo Jumatatu) Songea Vijijini ambapo lori lilikuwa limebeba shehena petroli na likiendeshwa na Hubert Mpete ambaye bado hajajulikana alipo. Lori hilo liliacha njia na kuingia porini kisha kugonga mti na kuwaka moto, na kichwa (cabin) kiliungua chote,” alisema Marwa.
Ajali hiyo imetokea ikiwa ni siku mbili tu tangu ajali kama hiyo itokee juzi, Jumamosi, maeneo ya Itigi, Msamvu mjini Morogoro na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 70 huku wengine zaidi ya 50 wakijeruhiwa vibaya kwa moto uliolipuka kutokana na mafuta ya petroli.
Imeelezwa kuwa katika ajali hii ya leo kule Ruvuma, wananchi wamekimbia na kubadili njia ili yasiwapate kama yaliyotokea Morogoro.
Taarifa zaidi tutaendelea kuwajuza.