Daktari Bigwa na Mkufunzi Mkuu wa Huduma ya Tiba ya upasuaji wa Watoto kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu cha Elexandria Nchini Misri Saber M.Waheeb akitoa maelezo kwa Waandishi wa Habari kuhusu lengo lililowaleta Zanzibar huko Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume.
Daktari kutoka Idara ya Upasuaji wa Watoto katika Hospitali ya Mnazi Mmoja Mwanabaraka Saleh Haji akitoa maelezo kwa Waandishi wa Habari huko Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume kuhusu ujio wa Madaktari kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu cha Elexandria Nchini Misri.
Mkurugenzi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Zanzibar Balozi Mohamed Haji Hamza (Kulia) akitoa maelezo kwa Waandishi wa Habari kuhusu uhusiano uliopo na Hospitali ya Chuo Kikuu cha Elexandria Nchini Misri.
Picha ya pamoja wakiwemo Madaktari Bigwa wa Upasuaji wa Watoto kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu cha Elexandria Nchini Misri pamoja na Wenyeji wao kutoka Zanzibar.
Picha na Maryam Kidiko – Maelezo Zanzibar.
*******
Jumla ya madaktari bingwa wanane kutoka Chuo Kikuu cha Alexandria Nchini Misri wamewasili Zanzibar na wanatarajia kufanya upasuaji wa watoto katika Hospital ya Mnazi Mmoja.
Akizungumza na Waandishi wa habari huko Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume baada ya mapokezi ya Madaktari hao Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mohamed Haji Hamza amesema kila mwaka hufika kambi ya madaktari hao kufanya huduma ya upasuaji kwa watoto.
Akielezea huduma hizo zitazotolewa kwa Watoto wanaolazwa katika Hospital ya Mnazi mmoja ni wale wasiokuwa na sehemu ya kutoka haja kubwa na kukosekana kwa tundu ya kufanyia haja ndogo.
Pia ameeleza kuwa zaidi ya watoto mia mbili wamefanyiwa upasuaji toka walivyoanza kuja mara ya kwanza 2013 hadi kufikia hivi sasa ambapo ni muendelezo wa huduma hiyo kupitia juhudi za Serikali kuwasogezea wananchi matibabu karibu.
Hivyo amesema mara hii wanatarajia kufanya upasuaji wa watoto 50 wenye matatizo hayo pia Chuo hicho kina mashirikiano na Hospital ya Muhimbili, Mnazi mmoja pamoja na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) .
Akitoa wito kwa jamii Balozi Hamza amewataka kuitumia vyema fursa hiyo kwa kuwaleta watoto wenye matatizo ili kufanyiwa huduma hiyo ambayo hutolewa bure huko Hospitali Kuu ya Mnazi mmoja .
Nae Daktari kutoka Idara ya Upasuaji ya Watoto kutoka Hospitali ya Mnazi Mmoja Mwanabaraka Saleh Haji amesema madaktari hao watakuwepo kwa muda wa siku tatu kwa lengo la kutoa matibabu yaliyokusudiwa.
Vile vile amesema lengo la madaktari hao kuja Zanzibar ni kufanya upasuaji kwa pamoja na madaktari wa hapa ili waweze kupata taaluma zaidi.
Kwa upande wake Daktari bingwa na Mkufunzi Mkuu wa huduma ya tiba ya upasuaji wa watoto kutoka Chuo Kikuu cha Alexandria Nchini Misri Dr Saber M. Waheeb amesema ujio wao unatokana na urafiki uliopo na kufanya kazi kwa pamoja ili kukuza udugu uliopo .