Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima (wa pili kulia) akiangalia namna dhahabu inavyochenjuliwa na Bi. Mary Matiko Makorere kwa kutumia zebaki katika eneo la wachimbaji wadogo katika wa Mtaa wa Kebaga, Kata ya Kenyamanyori Wilayani Tarime. Serikali imeazimia kupunguza matumizi ya zebaki kwa wachimbaji wadogo kutokana na athari kwa binadamu na mazingira.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima akizungumza na wakazi wa Mtaa wa Kebaga, Kata ya Kenyamanyori Wilayani Tarime, Mkoa wa Mara ambao wanajishughulisha na shughuli za uchimbaji madini na kuchenjua dhahabu kwa kutumia zebaki. Naibu Waziri amewaeleza athari za matumizi ya zebaki na kuwataka kujiunga na vikundi rasmi ili waweze kunufaika na mikopo itolewayo na Serikali.
Mjiolojia kutoka Mkoa wa Mara Bw. Solomoni Mwambeje (kushoto) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mussa Sima mara baada ya kutembelea mtambo maalumu wa kuchenjua dhahabu wa Kakulilo Tarime Mkoani Mara.
……………………….
Na Lulu Mussa,Tarime
Serikali imeandaa Mpango-Kazi wa Taifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu ambao umeainisha fursa mbalimbali zitakazowezesha sekta ya wachimbaji wadogo kuendelea na shughuli za uzalishaji wa dhahabu bila kuathiri sekta ya Mazingira nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima mara baada ya kufanya ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za hifadhi na usimamizi wa mazingira katika Wilaya ya Tarime Mkoani Mara hususan maeneo ya wachimbaji wadogo wa dhahabu.
Amezitaja fursa hizo kuwa ni pamoja na Upatikanaji wa masoko ya Dhahabu kupitia masoko ya madini ya mikoa yanayojengwa katika mikoa yote nchini; Upatikanaji wa mikopo midogo na ya kati kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu na Kuwezesha vikundi vya kinamama wanaojishughulisha na uchimbaji wa dhahabu kwa kutoa mafunzo kuhusu uchenjuaji salama na rafiki kwa mazingira na mikopo.
Naibu Waziri amesema Ofisi yake inaendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu kuhusu madhara ya zebaki kwa afya ya binadamu na mazingira na kuwataka wachimbaji wadogo kuchenjua dhahabu kupitia vituo mahiri saba (7) vya mafunzo na uchenjuaji wa dhahabu vinavyojengwa katika mikoa ya Simiyu, Mara, Kagera, Katavi, Mbeya, Ruvuma and Tanga na Geita chini ya Wizara ya Madini.
Amesema, Serikali imeona umuhimu wa kuungana na jumuiya ya kimataifa ili kuweza kukabiliana na madhara yatokanayo na matumizi ya Zebaki katika uchenjuaji wa dhahabu kwa wachimbaji wadogo na kuwaelimisha kutumia katika njia salama na rafiki wa mazingira ikiwemo matumizi ya ”gloves” wakati wa ukamatishaji na matumizi ya vigida wakati wa uchomaji wa dhahabu ili kudhibiti athari za mvuke wenye zebaki unaotokana na uchomaji wa dhahabu.
Akiwa katika Kata ya Kenyamanyori Mtaa wa Kebaga Naibu Waziri Sima amepata fursa ya kujionea shughuli za uchenjuaji wa dhahabu kwa kutumia zebaki ambayo imebainika kuwa na athari kwa afya za binadamu na mazingira kwa ujumla.
Akizungumza na wakazi wa Mtaa wa Kebaga Naibu Waziri Sima amesema zebaki inasababisha magonjwa ya ngozi, Moyo, Figo na kuharibu mfumo wa neva za fahamu endapo watumiaji hawatazingatia miongozo iliopo.
“Sisi kama Serikali lengo letu kubwa ni kuhakikisha tunawaelimisha wananchi wetu kwa kuwaambia madhara ya matumizi ya zebaki na kuwashawishi kutotumia zebaki kwa shughuli za uchenjuaji dhahabu” Sima alisisitiza.
Amesema njia kuu ambazo zinaweza kusababisha binadamu adhurike na Zebaki ni kupitia ngozi hususan wakati wa uchenjuaji wa dhahabu; kuvuta mvuke wa Zebaki; na kunywa maji na kula vyakula vilivyochafuliwa na Zebaki kwa kuwa hudumu katika mazingira kwa muda mrefu.
Zebaki ni metali pekee iliyo katika hali ya kimiminika ambayo hutumika katika sekta ya afya katika vifaa tiba, tiba ya meno na uhifadhi wa chanjo; uzalishaji viwandani kama vile vipodozi, viutatilifu na bidhaa mbalimbali ikiwemo betri, swichi, taa za umeme; na madini katika uchenjuaji wa dhahabu kwa wachimbaji wadogo.