Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza na wachimbaji wadogo (hawapo pichani) wa madini katika ukumbi wa mkutano wa Uvinza alipofanya ziara ili kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi tarehe 29/July, 2019.
Waziri wa Madini, Doto Biteko akisikiliza jambo kutoka kwa wachimbaji walioshiriki mkutano baina yake na wachimbaji wadogo wa Madini wa Uvinza kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Bi. Mwanamvua H. Mrindoko.
Wachimbaji wadogo wa Madini Uvinza, wakimsikiliza waziri wa Madini Doto Biteko (hayupo pichani) wakati wa kikao baina ya waziri Biteko na wachimbaji wadogo wilayani Uvinza mkoani Kigoma.
Afisa Madini Mkazi wa Kigoma akitoa taarifa fupi ya madini wakati wa Mkutano baina ya Waziri wa Madini Doto Biteko na wachimbaji wadogo (hawapo pichani) wa madini katika ukumbi wa mkutano wa Uvinza alipofanya ziara ili kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi tarehe 29/July, 2019.
Meneja wa kiwanda cha chumvi cha uvinza Ben Mwaipopo wa kwanza kushoto na Meneja Mkuu wa kuwanda hicho Mukash Mamlani Wa pili kulia wakimwonesha kitu Waziri wa Madini Doto Biteko wa kwanza kulia alipokuwa akikagua shamba la chumvi la uvinza.
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Uvinza ukishirikiana na kiwanda cha chumvi cha Uvinza, pamoja na ofisi ya Madini Mkoani Kigoma kujadili namna ya kuanzisha soko la chumvi katika halmashauri hiyo.
Maelekezo hayo yametolewa kufuatia maombi ya wananchi wa halmashauri hiyo ya uvinza kulalamikia ukosefu wa soko la kuuzia bidhaa hiyo na kuiomba serikali kufanya utaratibu wa kufungua soko ili kuwawezesha kufanya biashara yao mahali salama.
Agizo hilo limetolewa tarehe 29 July, 2019 katika ofisi za Kiwanda cha Chumvi cha Uvinza mara baada ya Waziri Biteko na ujumbe alioambatana nao kuwasili kwa lengo la kuzungumza na uongozi wa kiwanda hicho ili kuweka sawa mambo mbalimbali yaliyowasilishwa na wananchi wakati wa mkutano baina ya Waziri Biteko na Wachimbaji wadogo pamoja na wananchi wa Uvinza.
Moja kati ya malalamiko yaliyomfikia waziri Biteko ni malipo duni ya ujira kwa wafanyakazi wa kiwanda hicho ambapo aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kujadili na kufikia maamuzi ya kuongeza ujira kwa wafanyakazi wa kiwanda hicho waliodai kulipwa ujira mdogo.
Aidha, Biteko aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kufanya marekebisho hayo mpaka ifikapo tarehe mosi mwezi Agosti, 2019 mara baada ya Kiwanda kufanya mahesabu na kujiridhisha juu ya kiasi kinachobaki baada ya kutoa gharama za uwekezaji kiongezwe katika malipo hayo ya ujira.
Akijibu hoja ya baadhi ya wananchi wa Uvinza waliolalamikia uongozi wa kiwanda hicho kuuza chumvi inayozalishwa kiwandani hapo hiyo bei kubwa inayowafanya walanguzi hao kupata faida kidogo, Biteko aliutaka uongozi wa kiwanda hicho na wachimbaji wengine wa chumvi wilayani humo kupunguza bei hiyo ili kuiwezesha jamii inayowazunguka kunufaika na uwepo wa chumvi katika mji wao.
Biteko aliutaka uongozi wa kiwanda cha chumvi kuwapa wananchi sababu ya kuwapenda kwa kuwatendea mema. Aliendelea kwa kusema mtu mwenye kurekebisha bei ya chumvi kwa manufaa ya wafanyabiashara wadogo ni mwekezaji mkubwa. “ifanye jamii hii iugue siku ukiwa haupo, Ifanye jamii ikukumbuke kwa mema yako” Biteko alisisitiza .
Pamoja na hayo Waziri Biteko, aliutaka uongozi wa Halmashauri ya Uvinza, Ofisi ya Madini ya Mkoa wa Kigoma pamoja na uongozi wa kiwanda kukutana na kujadili namna na mahali patakapofaa kwa ajili ya kuanzisha soko la madini ili kuwaondolea adha ya soko la chumvi wananchi wa Uvinza.
Kufuatia malalamiko ya wananchi wa Uvinza ya kutozwa kiasi cha Tzs 500 ya ushuru kwa kila kilo 25 za chumvi, Waziri Biteko aliiagiza halmashauri ya Uvinza kufuta tozo hiyo na kueleza kuwa tozo hiyo haipo chini ya mamlaka yake na hivyo haitambui.
Akijibu kero ya mwananchi wa uvinza aliyejulikana kwa jina la Yona William Gwagula kwa niaba ya wanakikundi wa Twikome Salt Kinyo Chakuru juu ya watu waliokuwa wakiwatoza kodi kwa madai kuwa leseni iliyokuwa ikichimbwa na wanakikundi hao ni ya kwao jambo lililobainika kuwa si kweli, Waziri Biteko alimtaka Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kigoma David William Ndosi, kuifuta leseni hiyo mara moja na kuwapa wachimbaji hao wadogo ili waweze kuendeleza shughuli zao.
Kwa upande wake, Katibu wa Wachimbaji Wadogo wa Wilaya ya Uvinza, Hamisa Omari Kambi akiwasilisha changamoto wanazokumbana nazo alisema ni pamoja na maeneo yao kuvamiwa, ukosefu wa vitendea kazi, halmashauri kutowapa kipaumbele wamiliki wa leseni kwenye tenda za Serikali pamoja na kuomba kurahisishwa kwa utolewaji wa vibali vya kusafirisha Madini nje ya nchi ambapo changamoto zote zimepatiwa ufumbuzi.
Waziri Biteko atakuwepo Mkoani Kigoma kwa ziara ya siku mbili ambapo atafanya majadiliano na ofisi ya Mkoa wakishirikiana na Ofisi ya Tume ya Madini ili kujadili namna bora ya kuimarisha soko la Madini litakalowezesha kuweka mazingira rafiki na salama kwa ajili ya nchi jirani ya Kongo, kutokana na kuonesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika biashara ya Madini kupitia masoko yaliyoanzishwa hususani mkoani Kigoma.