Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akizungumza na
Wananchi wa Kijiji cha Namalebe, Kata ya Chitengule, Jimbo la Mwibara,
Wilayani Bunda Mkoa wa Mara, leo. Lugola amewataka wananchi nchini
wawe na utamaduni wa kushirikiana na Serikali kujenga shule, zahanati,
vituo vya polisi katika maeneo wanayoishi kuliko kuwa na akili potofu
miradi hiyo inajengwa na Serikali pekee. Picha na Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akibeba tofali kwa ajili
ya ujenzi wa Shule ya Msingi Ibwagulilo, ikiwa ni kuwahamasisha wananchi
wa Kijiji cha Namalebe, Kata ya Chitengule, Jimbo la Mwibara, Wilayani
Bunda Mkoa wa Mara, kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo mpya. Picha na
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akikagua mradi wa
ujenzi wa Shule ya Msingi Ibwagulilo, iliyopo Kijiji cha Namalebe, Kata ya
Chitengule, Jimbo la Mwibara, Wilayani Bunda Mkoa wa Mara. Lugola
amewataka wananchi nchini wawe na utamaduni wa kushirikiana na
Serikali kujenga shule, zahanati, vituo vya polisi katika maeneo wanayoishi
kuliko kuwa na akili potofu miradi hiyo inajengwa na Serikali pekee. Picha
na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
***************
Na Felix Mwagara, Mwibara (MOHA)
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amewataka wananchi
nchini wawe na utamaduni wa kushirikiana na Serikali kujenga shule,
zahanati, vituo vya polisi katika maeneo wanayoishi kuliko kuwa na akili
potofu miradi hiyo inajengwa na Serikali pekee.
Lugola ameyasema hayo wakati akikagua miradi mbalimbali ya maendeleo
jimboni kwake Mwibara, Wilaya ya Bunda, Mkoani Mara, leo, ambapo pia
alishirikiana na wananchi wa Kijiji cha Namalebe kushiriki ujenzi wa shule
mpya ya msingi ya Ibwagulilo iliyopo katika Kata ya Chitengule jimboni
humo ambayo Serikali imetenga shilingi milioni 96 kwa ajili ya kuikamilisha
shule hiyo.
“Mradi huu unaendelea vizuri, ambapo Serikali imetupa milioni 96.9
kuukamilisha mradi huu, nami nipo hapa na nimeshirikiana na wananchi
wangu kujitolea kujenga shule hii ambayo itawasaidia wananchi wa Kata hii
ili Watoto wao waweze kupata elimu,” alisema Lugola.
Waziri Lugola pia aliwahamasisha wananchi hao kushiriki matukio ya
maendeleo, pia alitoa mabati, saruji, nondo kwa ajili ya ujenzi wa zanahati,
na kuongeza madarasa katika shule mbalimbali zilizopo katika jimbo lake.
Naye Fundi Mkuu wa Shule ya Msingi, Marco Malima, alimshukuru Waziri
huyo kwa kufika katika eneo la ujenzi huo na imewapa nguvu zaidi
kufanikisha ujenzi huo kwa wakati.
“Fedha na vifaa kukamilisha ujenzi huu zipo, ujenzi huu ulianza mwezi mei
mwaka huu na unatarajiwa kukamilika mwezi wa saba mwaka huu,
ambapo tunajenga madarasa, nyumba za walimu pamoja na vyoo,”
alisema Malima.
Waziri Lugola anaendelea na ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo
jimboni humo pamoja na kuzungumza na wananchi na kutatua kero zao
zinazowakabili.
Lugola amewataka wananchi wa jimbo lake, waendelee kumuamini na
kushirikiana naye wakati wanahakikisha jimbo hilo linakua jipya zaidi
kimaendeleo.