Mwanariadha Matiko Nyamaraga (289) kutoka mkoa wa Mara akimaliza mbio za mita 400 na kufanikiwa kushika nafasi ya kwanza. Nyuma yake ni Dotto Mwandu wa Simiyu (533) na Steven Stephano wa Tabora aliyeshika nafasi ya tatu.
Mkimbiaji Nyairabu Chacha kutoka mkoa wa Mara akimalizia mbio za kupokezana vijiti mita 4 x 400 na kufanikiwa kushinda medali ya dhahabu leo katika viwanja vya chuo cha ualimu Mtwara
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Elimu Mhe.Mwita Waitara akizungumza na walimu na wanafunzi wanaoshiriki michezo ya UMITASHUMTA kutoka mkoa wa Mara wakati Mhe.Waitara alipotembelea viwanja vya chuo cha ualimu Mtwara kuona maendeleo ya michezo hiyo jana.
Wanariadha kutoka mkoa wa Simiyu walioshiriki mbio za mita 400 x 4 wakiwa katika picha ya pamoja na makocha wao mara baada ya kufanikiwa kushinda mbio hizo na kujinyakulia medali za dhahabu leo asubuhi katika viwanja vya chuo cha ualimu Mtwara
***************
Na Mathew Kwembe, Mtwara
Wanariadha kutoka mkoa wa Mara wametamba katika mbio za mita 400 zilizofanyika leo asubuhi kwenye viwanja vya chuo cha ualimu Mtwara baada ya kufanikiwa kuchukua medali za dhahabu kwenye mbio za mita 400 wavulana, na mbio za kupokezana kijiti mita 4 x 400 kwa wasichana, huku mkoa huo ukishika nafasi ya pili kwa mbio za mita 400 wasichana na kushika nafasi ya tatu kwenye mbio za kupokezana kijiti 4 x 400.
Mwanariadha Matiko Nyamaraga alifanikiwa kushinda medali ya dhahabu katika mbio za mita 400 baada ya kutumia muda wa sekunde 55:28, huku nafasi ya pili ikichukuliwa na Doto Mwandu wa Simiyu aliyetumia muda wa sekunde 55:50, huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na mkimbiaji Steven Stephano wa Tabora ambaye alitumia muda wa sekunde 55:72 na hivyo kufanikiwa kujishindia medali ya shaba.
Katika mbio za kupokezana vijiti wasichana, mkoa wa Mara ulijishindia nafasi ya kwanza baada ya wanariadha wake Zainabu Chacha, Anjelina Olembe, Nyanzobe Bahi na Nyairabu Chacha kufanikiwa kukimbia kwa kupokezana vijiti na kutumia muda wa dakika 4:18:97 na kuwashinda wanariadha kutoka mikoa mingine. Nafasi ya pili ilichukuliwa na wanariadha kutoka mkoa wa Mwanza ambao kwa jumla walitumia muda wa dakika 4:20:91 na walioshika nafasi ya tatu Simiyu walitumia muda wa dakika 4:21:69.
Mkoa wa Mara ulishika nafasi ya pili kwa upande wa mbio za mita 400 wasichana baada ya mkimbiaji wake Angelina Olembe kushika nafasi ya pili ambaye alitumia muda wa dakika 1:01:85, huku aliyeshinda mbio hizo Lucia Nestory wa Mwanza ambaye alishika nafasi ya kwanza baada ya kutumia muda wa dakika 1:01: 80. Nafasi ya mshindi wa tatu ilichukuliwa na mwanariadha Johari Hussein wa Tabora ambaye alitumia muda wa dakika 1:02:22.
Kwa upande wa mbio za kupokezana vijiti wavulana mkoa wa Mara ulishika nafasi ya tatu kufuatia wanariadha wake Matiko Nyamaraga, David Paul, Josephat Maranya na Daniel Maiko kutumia muda wa dakika 3:53:45. Nafasi ya kwanza ilichukuliwa na wanariadha kutoka mkoa wa Simiyu ambao walitumia jumla ya dakika 3:51:88 huku nafasi ya pili ikienda kwa wanariadha wa mkoa wa Mwanza ambao walitumia muda wa dakika 3:52:12.
Katika mchezo wa kurusha mkuki wavulana Pascas Qurejo wa Manyara alifanikiwa kujishindia medali ya dhahabu baada ya kurusha mkuki umbali wa mita 47 na sentimita 03, nafasi ya pili ilichukuliwa na Omary Abdallah wa Pwani ambaye alirusha umbali wa mita 38 na sentimita 93, na nafasi ya tatu ilichukuliwa na Bernard William wa Pwani ambaye alirusha umbali wa mita 38 na sentimita 67.
Mashindano hayo yanatarajiwa kumalizika tarehe 3 julai, 2019 ambapo yanatarajiwa kufungwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo katika uwanja wa Nangwanda mjini Mtwara.