Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), CP. Diwani Athumani akiwa pamoja na Balozi wa Uswizi nchini Tanzania Bi. Florence Mattli wakiwa pamoja kuzungumza na wanahabari katika uwasilishwajiwa mradi wa maadili kupitia filamu ya Bahasha.
NA EMMANUEL MBATILO
Inakadiriwa wananchi Zaidi ya 9,000 wamepata fursa ya kuona filamu ya Bahasha na kujifunza kutokana na maudhui yaliyomo yatokanayo na vitendo vya Rushwa.
Ameyasema hayo Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), CP. Diwani Athumani katika utoaji taarifa kuhusu Mradi wa Maadili kupitia Filamu ya Bahasha.
Akizungumza na Wnahabari Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi huyo amesema kuwa wao kama TAKUKURU wamekuwa washiriki wakubwa kwenye maandalizi na utekelezaji wa mradi huo tangu ulipoanza mwaka 2016.
“Sanjari na kushiriki kwenye maandalizi ya script ya filamu ya Bahasha ili kuongoza maudhui yake yashabihiane na uhalisia na sheria za nchi , Takukuru ilipeleka maafisa wake wane kwa nyakati tofauti wakati wa matukio ya kurekodi filamu hii yaliyofanyika jijini Arusha”. Amesema CP. Athumani.
Aidha, CP. Athumani ameongeza kuwa kutokana na umuhimu wa elimu itakanayo na filamu ya Bahasha, Ubalozi wa Uswizi nchini Tanzania na Takukuru walikubaliana kwamba watumie mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu wa 2019 katika kuhakikisha filamu hiyo inaonyeshwa wakati wa usiku wa mkesha wa Mwenge wa Uhuru.
“Maonyesho haya ya filamu yataendelea hadi usiku kwa kuamkia kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru 2019 yaani Oktoba 13, 2019”. Ameongeza CP. Athumani.
CP. Athumani amemaliza kwa kumshukuru Balozi wa Uswizi nchini Tanzania Bi. Florence Mattli kwa ushirikiano aliouonyesha katika mapambano dhidi ya Rushwa kwa kipindi chote ambacho amekuwa balozi hapa nchini na kumtakia mafanikio katika majukumu yake mapya baada ya kuachana na ubalozi wa Uswizi nchini Tanzania.
Kwa upande wake Balozi wa Uswizi hapa nchini ambao pia wamekuwa na msaada mkubwa katika kuhakikisha vitendo vya Rushwa vinatokomezwa Bi. Florence Mattli amesema kuwa filamu ya Bahasha itakuwa moja ya njia ya kutoa elimu kuhusu vitendo vya Rushwa hivyo wengi wataipokea elimu hiyo na kuifanyia kazi.
“Kila mtu anajukumu la kuhakikisha anatokomeza Vitendo vya Rushwa na tukifanya hivyo tutaondokana au kupunguza vitendo hivyo”. Amesema Bi. Frolence.