Home Mchanganyiko Viongozi wa Hospitali za mikoa ya Manyara, Mtwara na Tanga wafanya ziara...

Viongozi wa Hospitali za mikoa ya Manyara, Mtwara na Tanga wafanya ziara ya mafunzo ya kikazi katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete

0

Viongozi wa Hospitali za mikoa ya
Mtwara, Manyara na Tanga wakimsikiliza Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof.
Mohamed Janabi (hayupo pichani) wakati wa ziara yao ya
kikazi ya mafunzo ya siku tatu waliyoifanya katika Taasisi
hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiongea
na viongozi wa Hospitali za mikoa ya Mtwara, Manyara
na Tanga wakati wa ziara yao ya kikazi ya mafunzo ya
siku tatu waliyoifanya katika Taasisi hiyo.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiwa
katika picha ya pamoja na viongozi wa Hospitali za
mikoa ya Mtwara, Manyara na Tanga mara baada ya
kumalizika kwa ziara yao ya kikazi ya mafunzo ya siku
tatu katika Taasisi hiyo. Picha na JKCI

****************

Na Mwandishi Maalum

21/06/2019

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
imeahidi kushirikiana na Hospitali za mikoa ya Mtwara,
Manyara na Tanga kwa kuwatuma wataalamu wake
kwenda kutoa huduma za matibabu ya kibingwa ya moyo
katika Hospitali hizo ili kusogeza huduma karibu zaidi na
wananchi.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji
wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi wakati akiongea
na viongozi wa Hospitali za mikoa ya Mtwara, Manyara na
Tanga waliofanya ziara ya kikazi ya mafunzo ya siku tatu
katika Taasisi hiyo.

Prof. Janabi alisema ziara ya viongozi hao imewasaidia
kujifunza na kujionea kwa macho huduma mbalimbali za
matibabu ya moyo zinazotolewa kwa wagonjwa
wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.

“Tutakuja kuwatembela katika Hospitali zenu, tutaona
huduma mnazozitoa na tutashirikiana kwa pamoja kutoa
huduma kwa wananchi. Taasisi yetu imekuwa ikienda
katika Hospitali mbalimbali za mikoa kutoa huduma za
matibabu ya moyo kwa wananchi kwa siku za mbeleni
nanyi mtakuwa miongoni mwenu”, alisema Prof. Janabi.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wenzake Mganga
Mfawidhi wa Hospitali ya mkoa wa Manyara Dk.
Catherine Magali aliishukuru Taasisi hiyo kwa kuwapokea
na kuwapongeza kwa huduma bora wanazozitoa kwa
wagonjwa wanaowatibu.

Dk. Magari alisema katika ziara hiyo wamejifunza jinsi ya
kuwajibika na kutoa huduma nzuri kwa mgonjwa hata
kama mtoa huduma halipwi chochote.

“Kuwepo kwetu kwa siku tatu katika Taasisi hii tumejifunza
na kujionea jinsi mgonjwa anavyopokelewa, kwenda
kulipia bili, kwenda kwa daktari, kufanyiwa vipimo na
kupewa dawa kwa wakati hakuna kuchelewa katika
kupata huduma. Nasi tutaenda kuyafanyia kazi haya
tuliyoyaona katika Hospitali zetu”, .

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Tiba
Shirikishi wa Taasisi hiyo Dk. Delila Kimambo
aliwashauri viongozi hao kuzingatia usafi katika
Hospitali zao na kuhakikisha huduma bora
zinatolewa kwa wagonjwa kwani hakuna mtu
ambaye anapenda kulipia huduma mbaya.

Dk. Delila alimalizia kwa kuwasihi viongozi hao
kuvitunza vizuri vifaa vya Hospitali zikiwemo
mashine vinavyotolewa na wafadhili ili viweze
kutumika muda mrefu kwa kutoa huduma kwa
wagonjwa.

Katika ziara yao ya mafunzo ya siku tatu viongozi
hao wa Hospitali za Manyara, Tanga na Mtwara
walitembelea maeneo mbalimbali ya Taasisi hiyo na
kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa.