******************************
Juni 17, 2019
Dar es Salaam
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwa kushirikiana na Center for Reproductive Rights kimewasilisha malalamiko kwa Kamati ya Wataalamu ya Haki na Ustawi wa Mtoto Afrika ((ACERWC)) kupinga kufukuzwa na kutengwa kwa wasichana wajawazito kutoka shule za umma nchini Tanzania. Malalamiko hayo yametolewa kwa niaba ya wanafunzi wa kike nchini Tanzania kwa madai ya kukiuka Mkataba wa Afrika juu ya Haki na Ustawi wa Mtoto na mikataba mingine ya haki za binadamu ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia.
“Kuwataka wasichana kufanyiwa vipimo vya ujauzito kinyume na ridhaa yao, kuwafukuza watoto shuleni mara baada ya kupata ujauzito na kuwazuia kurudi shule mara baada ya kujifungua ni uvunjifu wa haki yao ya msingi ya elimu na haki ya usawa bila ubaguzi,” amesema Evelyne Opondo, Mkurugenzi Mkuu wa Center for Reproductive Rights – Afrika.
Tanzania ina historia ndefu ya kutekeleza mipango ya kibaguzi dhidi ya wasichana wanaopata ujauzito wakiwa shuleni. Mnamo Juni 2017, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. John Magufuli aliamsha upinzani mkali kutoka kwa watetezi wa haki za binadamu ndani na nje ya Tanzania dhidi ya amri aliyotoa kukataza wanafunzi wanaopata ujauzito na kujifungua kutokuruhusiwa kuendelea na masomo.
“Wakati wanafunzi wote, wasichana na wavulana wanaweza kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kukatisha masomo yao; wasichana wanakabiliwa na changamoto zaidi kwa mujibu wa sheria za Tanzania. Wasichana wanaopata ujauzito wakiwa shuleni wana haki ya kupata elimu na wanapaswa kuungwa mkono ili kubaki shule “amesema Fulgence Massawe, Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho – Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu.
Juni 16, 2019 katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, jamii ya ulimwengu iliangazia changamoto zinazowakabili watoto katika bara la Afrika. Leo, tunachukua hatua kuitaka serikali ya Tanzania kuwajibika kwa kukiuka haki za wasichana na kuongezeka kwa mimba za utotoni nchini Tanzania. Kwa mujibu wa Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya (TDHS) wa mwaka 2015-2016, mwanamke mmoja kati ya wanawake wanne wenye umri wa miaka 15 hadi 19 tayari wana watoto (mama). Elimu ya uzazi haitolewi mashuleni na wanafunzi wanasema kwamba hawana taarifa za msingi juu ya namna ya kujikinga na ujauzito. Wengi wa wasichana wanapata mimba kwa sababu ya kubakwa. Mpaka sasa, hakuna mtaala wa kitaifa wa elimu ya uzazi Tanzania Bara.
Mnamo Septemba 2012, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, pamoja na Shirika la Taifa la Usaidizi wa Kisheria, walifungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania dhidi ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa niaba ya wasichana wa shule nchini Tanzania, wakidai kuwa kuwapima wasichana ujauzito kwa lazima na utekelezaji wa masharti ya Elimu ya mwaka 2002, Mwongozo unaotaka (Kuwafukuza na Kuwatenga Wanafunzi Shuleni), hukiuka masharti ya Katiba ya Tanzania, hasa, Ibara ya 13 ya Katiba inayotoa haki ya usawa bila ubaguzi. Mnamo Agosti 2017, karibu miaka mitano baada ya waombaji kufungua kesi, Mahakama Kuu ilifutilia mbali madai ya waombaji.
Mnamo mwaka 2013, Center for Reproductive Rights kilitoa chapisho lilipewa jina “Forced Out: Mandatory Pregnancy Testing and the Expulsion of Pregnant Students in Tanzanian” (Upimaji Mimba wa Lazima na Kufukuzwa Shule kwa Wanafunzi Wajawazito Tanzania) likionesha kwamba viongozi wa shule nchini Tanzania wanalazimika kuwafukuza wasichana wenye ujauzito shuleni. Chapisho hilo pia lilitanabaisha kuwa kila mwaka, wastani wa wanafunzi 8,000 wa kike huacha shule kutokana na ujauzito. Kulazimishwa kupima mimba ni ukiukwaji mkubwa wa haki za wasichana za faragha na uhuru.