Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ametangaza kupangwa kwa maeneo yote itakapopita reli ya Mwendokasi (SGR) ili shughuli zitakazofanyika katika wilaya na vijiji inapopita reli hiyo kwenda sambamba shughuli za kiuchumi za mradi wa reli hiyo.
Aidha, Lukuvi alisema wakati wa kupanga maeneo hayo hakuna mwananchi yeyote atakayenyang’anywa eneo lake bali maeneo hayo yatapangwa kimji na kuainishwa matumizi yake kama vile ujenzi wa Viwanda na Mahoteli hivyo kuwataka wananchi wanaotaka kufanya uendelezaji mdogo mdogo kusubiri mpango huo.
Waziri Lukuvi alisema hayo tarehe 18 Mei 2019 katika vijiji vya Kwala na Soga vilivyopo Kibaha mkoa wa Pwani alipozungumza na wananchi wa maeneo hayo kuwaelezea mpango wa Wizara yake kupanga na kupima maeneo yote inapopita reli ya SGR ili kuendana na fursa za kiuchumi za mradi wa reli hiyo.
” Wilaya na vijiji vyote reli ya SGR itapita ardhi yao itapangwa na wale wananchi walio kando ya reli itakapopita wasubiri wasiwe na wasiwasi ardhi ya maeneo yao itengenezewe mpango na muongozo kuhusiana na maeneo hayo utatolewa” alisema Lukuvi.
Alisema, lengo la serikali kupanga maeneo hayo ni kutaka mpango mzima wa uendelezaji ukanda wa kiuchumi katika maeneo hayo ufahamike kitaifa na kimataifa ili kuvutia wawekezaji watakaotaka kuja kuwekeza na kubainisha kuwa fedha kwa ajili ya mpango huo zishatengwa.
Aliwatahadharisha wananchi wa vijiji hivyo kutokubali kuanza kuuza maeneo yao kwa kuwa baada ya kupangwa kwa maeneo hayo thamani ya ardhi itapanda na tayari baadhi ya watu wajanja kutoka nje ya vijiji hivyo washaanza kutafuta maeneo kwa ajili ya fursa hiyo.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, si vyema kila wilaya ikawa na mpango wake wa uendelezaji maeneo itakapopita reli hiyo bali serikali inachotaka ni kuwa na mpango wa kitaifa utakaotoa muongozo kwa wilaya zote kusisitiza kuwa ardhi katika maeneo hayo itasimamiwa na wilaya husika.
” Tukiacha maeneo ya kandokando ya reli bila kupanga na kupima kutafanyika vitu vya ajabu reli hii ina faida kubwa hivyo lazima kupanga maeneo inakopita ili kwenda sambamba na shughuli za kiuchumi za maeneo hayo” alisema Lukuvi.
Kwa mijibu wa Lukuvi, kuna timu imeundwa kwa ajili ya Mpango wa Uendelezaji Ukanda wa kiuchumi katika eneo inakopita reli ya SGR na timu hiyo inashirikisha wadau kutoka sekta mbalimbali kama vile za Nishati, Uchukuzi, Reli na Mawasiliano lengo likiwa kuwa na mpango utakaokidhi mahitaji ya uendelezaji ukanda kiuchumi katika eneo linakopita reli ya SGR.
Mapema akiwa katika eneo inapojengwa Bandari Kavu kijiji cha Kwala Kibaha vijijini, Mkuu wa wilaya ya Kibaha Asumpta Mshana alimueleza Waziri Lukuvi kuwa wilaya yake ilipanga kuitumia fursa ya reli hiyo pamoja na Bandari Kavu katika eneo la Kwala kwa ujenzi wa Hoteli, Maduka makubwa (Malls) , Nyumba za kupangisha (Apartments) ili wale wote watakaoitumia bandari hiyo kutoka maeneo tofauti waweze kupata malazi.
Akiwa katika Kwa Kijiji cha Soga Waziri Lukuvi aliwaambia wananchi wa kijiji hicho kuwa, eneo lao lishapandishwa hadhi na kuwa Mji hivyo ujenzi holela hautaruhusiwa na hati miliki za ardhi zitakazotolewa eneo hilo ni miaka 99 na aliwataka wakazi wake kuitumia fursa ya reli ya SGR kujiendeleza kiuchumi.
Mbunge wa Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa alimueleza Waziri Lukuvi kuwa zoezi la kuandaa mpango katika maeneo hayo liende sambamba na uboreshaji miundo mbinu katika vijiji hivyo ili kuwawezesha watu watakaoenda katika maeneo hayo kutokumbana na changamoto kama vile barabara, maji na umeme.