Na Mwandishi Wetu Mihambwe
Watanzania wametakiwa kutokubali kuona nguzo za umoja wa kitaifa zilizojengwa na waasisi wa Taifa kina marehemu Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Abeid Karume hazivunjiki kwa kuruhusu udini, ukabila na ubaguzi wa kisiasa.
Msimamo huo umetolewa na Afisa Tarafa ya Mihambwe wilayani Tandahimba Gavana Emmanuel Shilatu katika mkutano wa hadhara uliofanyika katoka kijiji cha Namunda huku akiwataka wananchi kujiweka kando na masuala hayo.
Gavana Shilatu alisema suala la maisha na maendeleo ya Watu halihitaji kutazamana kwa misingi ya ukabila, asili, itikadi au rangi, kwani katiba na sheria za nchi haziruhusu .
“Tusitarajie kupata maendeleo bila kwanza kukemea kwa nguvu zote udini, ukabila na ubaguzi wa aina yeyote. Binadamu wote ni sawa mbele ya sheria.” Alisema Gavana Shilatu
Afisa huyo Tarafa alisema msingi wa kukua kwa maendeleo ya watu kiuchumi, kijamii na kiutamaduni ni watu wenyewe, kushirikiana, kujengeka upendo kati yao, kuheshimiana kufanya kazi pamoja.
“Watu Duniani wanauana kwa ajili ya kubaguana kwa ukabila, udini na ubaguzi. Nchi yetu ndiyo pekee Duniani inayojali thamani ya utu na heshima ya kila mmoja.
Katika mkutano huo wa hadhara ulihudhuliwa na Mtendaji Kata Kitama, wajumbe wa Serikali ya Kijiji cha Namunda, watumishi wa umma ngazi ya kata ya Kitama na Tarafa ya Mihambwe.