Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Prof.Shadrack Mwakalila akizungumza wakati alipokuta na wahariri jijini Dar es Salaam kuzungumzia mafanikio ya Chuo hicho ndani ya miaka mitano katika Serikali ya awamu ya tano.Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mahusiano cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Mwasu Sware akizungumza wakati Mkuu wa Chuo hicho, Prof.Shadrack Mwakalila alipokutana na wahariri wa vyombo vya habari ili kuzungumzia mafanikio ndani ya miaka mitano katika Serikali ya awamu ya tano.
Mkuu wa MNMA, Prof. Shadrack Mwakalila akipata picha ya pamoja na baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari baada kukutana nao na kuzungumzia mafanikio ndani ya miaka mitano katika Serikali ya awamu ya tano.
************************************
CHUO cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), kimetaja mafanikio kiliyoyapata katika kipindi cha uongozi wa miaka mitano ya Rais Dk. John Magufuli, ikiwemo kukamilisha ujenzi wa Bweni la wanafunzi.
Akizungumza na Wanahabari leo jijini Dar es Salaam Mkuu wa MNMA, Prof. Shadrack Mwakalila, alisema wakati wa uongozi wa serikali ya awamu ya tano, chuo hicho kimepitia mafanikio makubwa na kusababisha utolewaji wa taaluma bora chuoni hapo.
Alisema katika kipindi hicho, wamefanikiwa kujenga bweni linalojumuisha wanafunzi wa kike na kiume 720, tangu mwaka 2018 na tayari limeshaanza kutumika.
Profesa Mwakalila, alisema chuo hicho pia kimefanikiwa kuongeza idadi ya udahili kwa mwaka wa masomo 2014 hadi 2015 kutoka wanafunzi 1,570 hadi 8,043 Tawi la Kivukoni na wanafunzi 22 hadi 1,753 katika tawi la Karume, Zanzibar.
Alisema pia kimeongeza wahitimu kutoka 568 mwaka 2014 hadi 3,237 mwaka 2015, pia watumishi kutoka 168 hadi 285 na Wahadhili wenye Shahada ya Uzamili kutoka wawili hadi 35.
Aliongeza pia kimeongeza program za shahada kutoka tatu hadi 10, Shahada ya Uzamili moja, Stashahada 11 na Astashahada 11, huku mitaala yake ikiboreshwa kwa kuingiza masomo ya uongozi, maadili na utawala bora kwa taaluma zote.
Kwa mujibu wa Profesa Mwakalila, chuo hicho kimeongeza idadi ya vitabu 20,000 kwa ajili ya Maktaba za matawi yote na pia kimejenga ukumbi wa mihadhara wa kisasa unaochukua watu 300 kwa wakati mmoja.
Alisema chuo hicho kimefanikiwa kupeleka watumishi wake katika vyuo mbalimbali nje ya nchi kwa ajili ya kuwaendeleza kimasomo ambapo kwa kipindi hicho wamepeleka wanafunzi 40.
Aliongeza kuwa chuo hicho kimefanikiwa kutatua chnagamoto kubwa iliyokuwa ikikabiliana nacho, ambayo ni mmomonyoko wa udogo kutoka katika fukwe ya bahari ambapo sasa kimejenga ukuta na kufanikiwa kuzuia hilo.
“Pia tumeimarisha mahusiano mazuri ya kitaaluma na taasisi nyingine ili kuboresha tafiti na kupata maarifa ya mafunzo bora,” alisema.
Alisema kupitia idara ya TEHAMA, chuo hicho kimefanikiwa kutoa bunifu 22 kwa mwaka wa masomo 2019 hadi 2020 na kuwezesha wanafunzi watano kwenye mashindano ya ubunifu ambapo mwanafunzi wa MNMA amepata nafasi ya pili.
Aliongeza kuwa chuo hicho kimefanikiwa kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa maktaba itakayochukua wanafunzi 2,500 kwa ajili ya tawi la Kivukoni na Bweni la wanafunzi wa kike na kiume 1,568 kwa ajili ya tawi la Pemba.
Alisema mafanikio mengine ni kuanzisha tawi la chuo hicho Pemba, ili kupanua wigo wa utoaji wa elimu kama lilivyo lengo la kuanzishwa kwa chuo hicho.
Profesa Mwakalila, alisema hadi sasa wamefanikiwa kupata eneo jijini Dodoma kwa ajili ya kuanzisha tawi jipya.
Alisema maboresho yaliyofanywa na chuo hicho ndio msingi wa taaluma bora katika masuala ya uongozi, maadili na uzalendo yanayotolewa na chuo hicho kwa wanafunzi wa taaluma mbalimbali na hata watumishi wa sekta za umma na binafsi.
“Chuo chetu kimekuwa kikitoa mafunzo ya uongozi, uzalendo na maadili kwa wanafunzi wa taaluma zote kutokana na msingi wa kuanzishwa kwa chuo hiki,” alisema.