Home Uncategorized TAKUKURU MANYARA YAOKOA NA KUREJESHA SHILINGI 11,719,877.90

TAKUKURU MANYARA YAOKOA NA KUREJESHA SHILINGI 11,719,877.90

0

Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Isdory Kyando akizungumza na waandishi wa habari mjini Babati.

************************************

Na mwandishi wetu, Manyara

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Manyara, imefanikiwa kuokoa na kurejesha kiasi cha shilingi 119,719,877.90 kwa vyama vya ushirika, mikopo umiza na fedha zilizokuwa zinaelekea kufanyiwa ubadhirifu kwenye matumizi mbalimbali ya shughuli za Serikali.

Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Isdory Kyando ameyasema hayo akizungumza mjini Babati wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi kuanzia mwezi Julai hadi Septemba mwaka huu.

Kyando amesema fedha hizo zimerejeshwa moja kwa moja kutokana na maelekezo ya Rais John Magufuli juu ya ufuatiliaji wa fedha zote za vyama vya ushirika na kurejesha fedha ambazo zilikopeshwa na kuendelea kukaa nazo bila kuzirejesha kinyuma na utaratibu.

Amesema kati ya fedha hizo zilizookolewa na kurejeshwa kiasi cha shilingi 55,022,650 ni fedha za vyama mbalimbali vya ushirika na kiasi cha shilingi 25,750,787.90 zilirejeshwa serikalini kupitia akaunti ya TAKUKURU.

Amesema kiasi cha shilingi milioni 10 ni fedha za mwalimu mstaafu ambaye alidhulumiwa na wakopeshaji wadogo wadogo (mikopo umiza), baada ya kudhulumiwa shilingi 54,000,000.00 kwa kutozwa riba kubwa isiyo halali na kinyume na utaratibu.

“Pia, jumla ya shhilingi 17,016,440.00 zilirejeshwa kwa wananchi ambao walidhulumiwa haki zao katika mazingira mbalimbali,“ amesema Kyando.

 Amesema wamefanikiwa kuingilia kati na kuzuia ulipaji wa zaidi ya shilingi 12,000,00 kutokana na utata wa mkataba wa deni la shilingi 3,400,000 kwani kwenye uchunguzi wao walibaini kuwa mlalamikaji hakusaini mkataba huo kwa hiyari na miongoni mwa watoa mikopo umiza.

Amesema shilingi 6,530,000 zilirejeshwa kutoka kwenye ubadhirifu wa fedha za kisimacha maji cha NALANG`TOMON.

“Shilingi 400,000 zilirejeshwa kwa katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambazo ni fedha za michango ya wagombea ambao walitozwa kinyume na utaratibu,“ amesema Kyando.

Ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Manyara, kuendelea kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwani milango ya TAKUKURU ipo wazi kuwahudumia wakati wote.

Amesema wananchi wa mkoa wa Manyara na wajumbe wa Serikali za vijiji wafuatilie miradi ya maendeleo inayotekelezwa  kwenye maeneo yao na pale wanapoona mashaka ya utekelezaji huo watoe taarifa mara moja kwenye ofisi za TAKUKURU zilizo karibu nao.

“Viongozi wa ngazi mbalimbali kwenye Taasisi zote za mkoa wa Manyara, wahakikishe wanawasimamia watendaji walio chini yao ii kutoa huduma stahiki, kuhakikisha shughuli za maendeleo zinafanyika kwa ufanisi, tija na kwa wakati,“ amesema.

Amesema wananchi wa Manyara wajiepushe na wimbi la matapeli wanaowapigia simu na kujifanya ni maofisa wa TAKUKURU na wanawajulisha wimbi la watu hao bado lipo na mtu yeyote akipigiwa simu hiyo atoe taarifa TAKUKURU ofisini au kwenye namba 113.