******************************************
MTAALAMU wa Epidemiolojia na Udhibiti wa Magonjwa wa Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii ,Jinsia,Wazee na Watoto Dr.Azma Simba, ametoa rai kwa wataalam kuungana na kushirikiana ili kukabiliana na magonjwa ya milipuko na kuimarisha usalama wa afya duniani.
Dr.Simba ametoa rai hiyo wakati anawasilisha mada ya agenda ya kukabiliana na matukio muhimu ya kiafya ya kimataifa, kwenye mafunzo ya utayari wa kukabiliana na magonjwa mlipuko kwa timu za dharura kwa wataalam kutoka mikoa ya Ruvuma na Mtwara.
Akizungumza katika mafunzo hayo ambayo yamefanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Tiffany mjini Mtwara, Dr.Simba amesema dunia imeathirika zaidi na magonjwa ya milipuko yakiwemo ebola na COVID 19 na kwamba mwaka 2014 Agenda ya Afya Duniani ilianzishwa kwa lengo la kuhakikisha Dunia inakuwa salama kutokana na milipuko ya magonjwa hayo.
“Nchi nyingi duniani zimeweka jitihada kubwa katika kujilinda na magonjwa ya mlipuko,hata hivyo ni vema watalaam kufanya kazi kwa ushirikiano ili pawepo na usalama wa afya duniani’’,alisema.
Mtaalam huyo wa kudhibiti magonjwa amesema, kupitia agenda ya afya duniani,imetolewa miongozo na kanuni za kimataifa zinazoongoza kukabiliana na magonjwa ya milipuko.
Ameyataja madhumuni ya Agenda ya afya ya dunia kuwa ni kuwepo kwa mifumo ya afya ambayo imejikita kuzuia,kutambua mapema na kukabiliana na ugonjwa unapotokea na kwamba milipuko mingi ya magonjwa inayotokea inaweza kuzuilika kwa njia ya chanjo.
Hata hivyo ametoa rai kwa timu za dharura za kukabili magonjwa ya mlipuko katika ngazi za Halmashauri na Mkoa kufanya ufuatiliaji wa magonjwa kwa wakati na kutoa taarifa mapema katika ngazi husika.
Kwa upande wake Daktari wa mifugo Dr.Moses Ole Neselle kutoka Shirika la Chakula na Kilimo Duniani(FAO) akitoa mada kwenye mafunzo hayo,ameyataja magonjwa sita ya kipambele ambayo yanaambukiza kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu kuwa ni Kichaa cha mbwa ambacho kinatarajiwa kutokemezwa mwaka 2030.
Ameyataja magonjwa mengine kuwa ni homa ya bonde la ufa,kutupa mimba kwa wanyama,mafua ya ndege,kimeta na ugonjwa wa ebola na amesisitiza kuwa magonjwa hayatambui mipaka ya nchi hivyo ni vema wataalam wote kushirikiana kukabiliana na magonjwa hayo.
Amesema asilimia 50 ya magonjwa yote yanaambukizwa kupitia virusi na kwamba asilimia 60 ya magonjwa ya binadamu yanasababishwa na wanyamapori hivyo ameshauri kuwepo mpango mkakati wa kukabiliana na magonjwa hayo.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Profesa Rudovick Kazwala imesisitiza kuwa katika kutokomeza magonjwa ya mlipuko ni lazima wataalamu wafanye kazi kwa kushirikiana ili kutoa matokeo chanya.