Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally amefafanua sababu za viongozi wa Upinzani kuikejeli na kuitukana CCM.
Akizungumza na wazee Afisi Kuu Zanzibar, tarehe 05 Oktoba, 2020 pamoja na masuala mengine ameeleza kuwa,
“Wazee wangu tumetukanwa sana hatujajibu mapigo kwa Matusi, kwa sababu nidhamu ya Chama Chetu, inatutaka tuvumiliane kisiasa, tumeitwa majalala, tumeitwa mbwa, tumeitwa wajinga tumechonganishwa na kila kundi la jamii yetu.”
“Tumechonganishwa na viongozi wa dini, watumishi, wafanyabiashara, wakulima, tumechonganishwa na wajasiriamali, mpaka sasa tumechonganishwa na jumuiya ya kimataifa.”
Akieleza sababu za uchonganishi huo amesema ni kwa sababu CCM inao uwezo wa kuongoza nchi kulinganisha na vyama vingine.
“Tumechonganishwa na kila kundi la jamii yetu kisa tunauwezo wa kutawala nchi, ndio dhambi yetu, Chama kinanguvu ya kuunganisha watanzania ndio dhambi yetu, tunaviongozi wenye msimamo wa kulinda rasilimali za nchi hii ndio dhambi yetu, tumeapa kuulinda muungano wetu wa serikali mbili ndio dhambi yetu.”
Akitoa msimamo wa Chama katika kipindi hiki cha uchaguzi, ameeleza kuwa, maelekezo ya Mwenyekiti wa CCM na Mgombea Urais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ni kutokulipa kisasi na kutokujibu matusi kwa matusi, bali kujibu matusi kwa hoja.