Home Mchanganyiko DKT.MWINYI KUPAMBANA NA VITENDO VYA KIBAGUZI KATIKA JAMII ENDAPO ATAKUWA RAIS VISIWANI...

DKT.MWINYI KUPAMBANA NA VITENDO VYA KIBAGUZI KATIKA JAMII ENDAPO ATAKUWA RAIS VISIWANI ZANZIBAR

0
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk.Hussein Ali Mwinyi,akisalimiana na viongozi mbalimbali wa madhehebu ya kikiristo Zanzibar mara baada ya kuwasili katika ukumbi wa baraza la Sheikh Idrissa Abdulwakil kikwajuni katika mkutano na viongozi wa dini ya kikiristo.
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk.Hussein Ali Mwinyi,akizungumza na viongozi wa dini wa madhehebu ya kikiristo Zanzibar.
BAADHI ya waumini wa madhehebu ya dini ya kikiristo Zanzibar wakimsikiliza Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk.Hussein Ali Mwinyi, wakati wa mkutano wao na kiongozi huyo. 
********************************
PICHA DSC-1420 -(PICHA NA IS-KAKA OMAR ZANZIBAR)
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk.Hussein Ali Mwinyi,amesema endapo atakuwa rais wa Zanzibar atapambana na vitendo vyote vya ubaguzi wa aina mbalimbali uliopo katika jamii.
Alisema ili kuonfosha vitendo vya ubaguzi visiwani humo ni kukiri na kukubali kuwa vitendo hivyo vipo Kisha kuchukua hatua ya pili ya kuondosha vitendo hivyo.
Hayo aliyasema wakati akizungumza na viongozi na waumini wa madhehebu mbalimbali ya dini ya kikiristo Zanzibar,huko katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul Wakil Kikwajuni.
Alisema nchini Kuna ubaguzi wa dini,ubaguzi wa kijinsia,ubaguzi wa kikanda wa ubara,uunguja na upemba na yote hayo yanatakiwa kuondolewa.
Alisema changamoto hizo zikiondolewa Zanzibar inaimarika kwa kasi kiuchumi,kijamii na kisiasa.
Alieleza viongozi na waumini wa dini ni wadau wakubwa wa maendeleo hivyo wanatakiwa kutoa mchango wao katika maendeleo ya nchi.
Dk.Mwinyi,alisema lengo lake la kugombea ni kuwaletea wananchi wa makundi yote maendeleo endelevu.
Alisema dhamira yake ni njema ya kuwatumikia wananchi wote kwani kiongozi yeyote anayetafuta uongozi mkubwa wa nchi hawajibiki kwa wale wanaompigia kura tu bali anawajibika hata kwa Mungu.
Alisema katika uongozi wake atahakikisha anatenda haki kwa makundi yote.
Pia atasimamia haki ya kikatiba ya kuhakikisha kila mtu anapata Uhuru wa kuabudu dini anayoiamini ili nchi ibaki kuwa salama.
“Nia yangu ni kutenda haki kwa wote na naamini mwenyezi Mungu atazijaalia nitekeleze nia yangu kwa vitendo”,alisema Dk.Mwinyi.
Alitumia nafasi hiyo kujiombea kura na kuwaombea wagombea wote wa CCM ili Chama kishinde na kuendea kuongoza dola.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi,aliwambia waumini hao kuwa Dk.Hussein amekuwa kiongozi mwenye sifa kubwa ya uongozi uliotuka na mcha Mungu.
Alisema Mgombea huyo,ana Nia ya dhati ya kuwatumikia wananchi hivyo waumini hao na jamii zao wahakikishe wanaompigia kura nyingi za ndio yeye pamoja na viongozi wote wa CCM.
Alisema CCM itakuwa pamoja na wananchi wote wa makundi mbalimbali chini ya mfumo mpya wa Zanzibar mpya na Uchumi mpya.
“Chama Cha Mapinduzi kimemuamini na kumpa dhamana Dk.Hussein kwa kuamini kuwa ana sifa na vigezo vyote vya kutuvusha kuelekea kilele cha mafanikio ya kuijenga Zanzibar imara na yenye nguvu kiuchumi na kijamii”,alieleza Dk.Mabodi.
Nae Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Catherine Peter Nao amewambia waumini hao kuwa mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk.Hussein Ali Mwinyi ni mgombea mwenye sifa ya unyenyekevu,mbunifu na mchapakazi na yupo karibu na watu.
Kwa upande wake Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC) Christina Joram alizitaja changamoto zinazowakabili waumini wa kanisa hilo kuwa ni pamoja kuwepo kwa urasimu kwa waumini hao pindi wanapotaka kumiliki ardhi.
pia aliwataja baadhi ya wakuu wa mikoa,wakuu wa wilaya na masheha hawatoi ushirikiano kwa waumini hao.
Alisema Vijana wengi wasomi wa kikiristo bado hawajaajiriwa serikalini,hivyo dk.mwinyi akipata nafasi ya kuwa Rais ahakikishe kundi hilo linapata ajira.
Alishauri kuwa viongozi hao wamekiomba Chama kuachwa utamaduni wa kuwakumbuka viongozi hao kila ikifika uchaguzi hivyo kwa Sasa wahakikishe wanatengeneza mahudiano mapya ya kushirikiana. 
Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wakiristo Zanzibar Askofu Agostino Shayo amesema waumini hao ni watu wa amani na sio shari.
Alisema kuwa matukio yote yanayowakuta wakiristo hawalipizi kisasi kwani wao mafundisho yao yanawaongoza kuwa wavumilivu.
Amesema Dk.Mwinyi,akiwa rais awe mwanga wa kuleta haki kwa waumini hao kwani wamekuwa wakiishi kwa changamoto kubwa ambazo zimekuwa hazitatuliwi kwa wakati.
Alisema waumini hao hawaombi upendeleo bali wanaomba haki itendeke kwa waumini wote wa dini zilizopo nchini.
“Mwenyezi Mungu akikujaaliwa kuwa rais wetu wa Zanzibar ,tunaomba mungu akupe nguvu za kutatua changamoto zote zinazotukabili nasi tuishi Kama wanavyoishi waumini wa madhehebu mengine.”,alisema Askofu Shao.
Mkuu wa Jimbo Kuu la KKKT Kanda ya Zanzibar Mchungaji Shukru Maloda, alisema makanisa ya kikiristo yataendelea kuhubiri amani na kuwaelekeza waumini mambo mema.
Mkutano huo ni sehemu ya kampeni za kisayansi za CCM zinazoendeshwa hivi Sasa na mgombea huyo wa kiti Cha Urais Zanzibar kupitia CCM,ambapo wananchi wanafuatwa katika maeneo yao na kuzungumza changamoto zinazowakabili ili zitatuliwe na serikali ijayo ya awamu ya nane.