Mwalimu Majogolo Ngwalali katikati akiwa na Muuguzi mkuu wa wodi namba 2B Bi Furaha Godfrey (Kushoto ) pamoja na Mkuu wa kitengo cha Uhusiano MOI Bw. Patrick Mvungi (Kulia) baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali jana. (Picha na MOI)
**************************************
Na Mwandishi wetu
Mwalimu Majogolo Ngwalali (36) wa shule ya sekondari Kiagata Butiama mkoani Mara aliyejeruhiwa na mwanafunzi wa kidato cha tatu akiwa kazini ameishukuru Taasisi ya MOI kwa kumpatia matibabu mazuri kwa wakati.
Akizungumza baada ya kuruhusiwa kutoka MOI, Mwl Majogolo amewashukuru wahudumu wa Afya wote kwa kumpa huduma bora na sasa anaendelea vizuri .
“Kwanza ninawashukuru madaktari na wauguzi hapa MOI wamenuhudumia vizuri toka siku ile ya tarehe 24/09/2020 nilipofika hapa saa 6 usiku ,pili nashukuru wahudumu wa kituo cha Afya Kiagata na Hospitali ya Mara ambako nilipata huduma za awali kabla ya kuja MOI “,alisema Mwl. Majogolo.
Pia, ameishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Butiama ambayo ilihakikisha anapata huduma kwa wakati ikiwa ni pamoja na kumtafutia usafiri wa ndege kufika Dar s salaam.
Akisimulia namna alivyojeruhiwa Mwl. Majogolo, amesema alijeruhiwa na panga na mwanafunzi wa kidato cha tatu akiwa katika ukaguzi wa kawaida wa watoro na watorokaji.
“Tulikuwa tunafatilia watorokaji na watoro ndipo mwanafunzi wa kidato cha tatu alipo nijeruhi kwa kunikata mkono kwa panga “alisema Mwl. Majogolo .
Akizungumzia afya yake baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali Mwl. Majogolo amesema anaendelea vizuri sana tofauti na hapo awali ambapo alikuwa na maumivu makali .
“Namshukuru Mungu naendelea vizuri hapo awali nilikuwa na maumivu makali nilikuwa siwezi kuchezesha vidole vyangu lakini sasa hivi vinacheza.Hii inatia moyo sana “alisema Mwl. Majogolo.
Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha uhusiano MOI Bw. Patrick Mvungi amesema Mwl. Majogolo alipokelewa tarehe 24/09/2020 saa 6 usiku alipatiwa huduma ya upasuaji wa dharura siku hiyohiyo na sasa ameruhusiwa kurudi nyumbani kwani afya yake imeimarika.
“Tumemruhusu kwenda nyumbani kwani afya yake imeimarika na anaendelea vizuri atarudi baada ya wiki mbili jumanne kwenye kliniki zetu” alisema Mvungi.
Mwl. Majogolo alifanyiwa upasuaji mkubwa wa kurekebisha mishipa katika mkono wake wa kushoto ambao aliyojeruhiwa na mwanafunzi wa kidato cha tatu akiwa katika majukumu yake katika shule ya Kiagata Butiamma mkoani Mara.