……………………………………………………….
NA MWAMVUA MWINYI,BAGAMOYO
WAZIRI MKUU ,Kassim Majaliwa ameeleza uzalishaji wa sukari ya mezani nchini unafikia tani 380,000 ambapo bado kuna bakaa ya tani 70,000,hivyo kuna kila sababu ya kuongeza uzalishaji wa sukari kwa wingi na kilimo cha miwa ili kuondokana na kuagiza bidhaa hiyo nje ya nchi .
Aidha amewaelekeza maafisa kilimo waende wakatoe elimu kwa wananchi mjini Bagamoyo kuhusu kilimo cha miwa ,faida yake na kutoa uhakika wa soko ili wasisite kushiriki kwenye kilimo cha miwa .
Alitoa rai hiyo wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wa mkoa na wafanyakazi wa kiwanda cha sukari cha Bagamoyo, Makurunge mkoani Pwani, alipokwenda kukagua ujenzi wa kiwanda sanjali na miundombinu ya mradi wa shamba la miwa ikiwemo vitalu vya mbegu, miche, maabara ya kupima maji na udongo na miundombinu ya umwagiliaji.
Pamoja na hayo,Majaliwa aliridhishwa na kazi inayofanyika na kudai kukamilika kwa mradi huo kutahakikisha sukari inapatikana na kutoa fursa ya kilimo cha miwa kwa wakazi wa maeneo jirani.
“Mahitaji ya sukari nchini yamefikia tani 450,000 kwa sukari ya mezani,sukari ya viwandani ambayo inatumika kutengeneza soda, biskuti na pipi mahitaji yake ni tani 165,000 ambayo hapa nchini hatuizalishi, kwa hiyo inabidi tuiagize kutoka nje ya nchi.”
” Viwanda vilivyopo vya TPC, Kagera, Mtibwa, Kilombero, Manyara na Bagamoyo bado kuna maeneo ya kulima miwa huko Tarime na Kigoma. “Tunawaalika wawekezaji walime miwa na kuzalisha sukari zaidi.” alisisitiza Waziri Mkuu.
Pia Majaliwa ,aliwataka Watanzania wawe wazalendo na kubadilika kwa kujifunza kujivunia kilicho chao.
Waziri Mkuu alisema Rais Dkt. John Pombe Magufuli kutoa eneo hilo lenye hekta 10,000 kwa mwekezaji Bakhresa ili lilimwe miwa na kujenga kiwanda cha sukari, ulilenga kuongeza uzalishaji wa sukari nchini.
Awali mkurugenzi wa Makampuni ya Bakhresa,Abubakar Bakhresa alimshukuru Rais Magufuli kwa kuwapatia eneo hilo .
Mkurugenzi wa Mahusiano wa Makampuni ya Bakhresa, Hussein Sufian alisema gharama ya mradi huo ni dola za Marekani milioni 100 nahadi sasa wameshapata asilimia 70 ya mtaji.
Alisema wameshatoa ajira kwa watu 600 ambapo 500 kati yao wanatoka kwenye vijiji jirani vinavyozunguka eneo la mradi na kwamba mara baada ya awamu ya kwanza kukamilika, uzalishaji utakapoanza wataweza kuajiri watu 1,500.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, alifafanua zao la korosho limewaingizia wakulima shilingi bilioni 60 kwa mwaka 2019,zao la ufuta liliwaingizia shilingi bilioni 19,sasa wanatekeleza uanzishwaji wa zao la mkonge, kwa hiyo kilimo cha miwa kimekuwa zao la nne na kata tano zipo tayari kulima miwa.