Home Mchanganyiko WALIOCHUKUA HELA KWA WANANCHI ZA URASIMISHAJI NA HAWAJAKABIDHI KAZI MATATANI

WALIOCHUKUA HELA KWA WANANCHI ZA URASIMISHAJI NA HAWAJAKABIDHI KAZI MATATANI

0


 Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bibi Mary Makondo akisisitiza mikakati ya Wizara katika ukwamuaji wa kero za urasimishaji makazi holela nchini, zoezi linalotekelezwa na makampuni ya watu binafsi kwa asilimia kubwa. Malalamiko ya kazi za urasimishaji yamekuwa mengi sana kiasi cha kuichafua taswira ya Wizara kwa hiyo ni lazima kero hizo zitatuliwe sasa kwa namna yeyote ile.

Bibi Mary Makondo, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi akitoa rai kwa makampuni ya upangaji na upimaji (hayupo pichani) yanayoendesha la urasimishaji jijini Arusha wakati alipokutana nao na kukitambulisha kikosi kazi cha kukwamua kero za urasimishaji jijini huko. Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro Bwn. Huruma Lugala ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Wapima Ardhi Tanzania, akitoa ufafanuzi juu ya vigezo vinavyohitajika ili kampuni isajiliwe na kupewa mradi wa kufanya kazi ya upimaji. Lugala alisema kuna mambo mengi ya kuangalia ikiwa ni pamoja na masuala ya nidhamu katika kazi kwa ajili ya kujenga uaminifu kati ya Kampuni, wananchi na Serikali. Wamiliki na wawakilishi wa makampuni mbalimbali yanayofanya kazi za urasimishaji jijini Arusha wakifuatilia kwa makini mada kuhusu mikakati ya kukwamua kero za urasimishaji kutoka kwa kiongozi wa kikosi kazi maalum cha kukwamua kero hizo (hayupo pichani) kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Arusha Bwn Leo Komba akielezea hali ya
urasimishaji ilivyo katika mkoa wake kwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, wakati
alipokutana na makampuni yanayofanya kazi ya urasimioshaji katika mitaa 120 ya jiji la Arusha. Praygod Shao, kiongozi wa kikosi kazi maalum cha ukwamuaji kero za urasimishaji kilichoundwa na Wizara ya Ardhi akitoa ufafanuzi juu ya utekelezaji wa mkakati wa
kikosi kazi hicho katika kufikia malengo ya kukwamua kero zote za urasimishaji. Shao
alisema, lengo la Serikali lilikuwa nzuri kuamua kufanya kazi za urasimishaji na wadau
wa sekta binafsi kwa hiyo ni lazima sera na miongozo itumiwe vizuri ili kazi hizo ziwe na
tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

……………………………………………………………

Na E.L. Solla – Arusha

Makampuni ya watu binafsi yanayofanya kazi za urasimishaji katika mitaa mbalimbali ya
jiji la Arusha yameagizwa kukamilisha kazi zao zote ifikapo Agosti 30 mwaka huu 2020,
vinginevyo Serikali haitawafumbia tena macho hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi
yao.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi Bibi Mary G. Makondo alipokutana na makampuni hayo jijini humo na
kuwaeleza mikakati ya Wizara katika kukwamua kero za urasimishaji, zoezi ambalo
linatakiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Agosti, 2020.

‘Serikali inapotoa miongozo ni lazima isimamiwe na itekelezwe ipasavyo.
Unaposhindwa kusimamia mkataba wako katika kutoa huduma unakosa uaminifu.
Kufanya kazi kwa kusimamia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ni kuwekeza kwa
yule aliyekupa hiyo kazi na kwa Serikali iliyokuamini na kukupa fursa, alisema Bibi
Mary.’

Aliongeza kwamba, lengo la Wizara kuanzisha urasimishaji lilikuwa ni kupandisha hadhi
na kuondoa makazi holela kwenye maeneo yaliyokwisha endelezwa tayari lakini, kazi
hii ilipaswa kuwa na ukomo na siyo kazi endelevu. Zoezi hili lilipaswa lifanyike kwa
malengo maalum na matunda yake yaonekane.

Katika jiji la Arusha pekee, kuna jumla ya makampuni 25 yanayofanya kazi za upangaji
na upimaji katika mitaa 120. Kati ya mitaa hiyo yote, hakuna mtaa hata mmoja ambao
kazi za urasimishaji zimekamilika licha ya kwamba wananchi wamechangia hela zao
kwa ajili ya kurasimishiwa maeneo yao. Hali hiyo ndiyo inayopelekea Serikali kupitia
wizara ya Ardhi kuchukua hatua za ziada kuona ni kwa namna gani kero hizo zinaweza
kukwamuliwa.

Awali, akizungumza na makampuni hayo yanayorasimisha makazi holela katika jiji la
Arusha Kamishna Msaidizi mkoa wa Arusha Bwn Leo Komba alisema; utendaji kazi wa
makampuni hayo hauridhishi, wamesababisha malalamiko mengi sana kutokana na
kazi zao kutokukamilika kwa wakati. Aliongeza kwamba, makampuni mengi yanapitamitaani kuhamasisha wananchi kulipia gharama za urasimishaji na fedha hizo
wanachukua lakini kasi ya kuwapimia ili wamilikishwe ni ndogo sana.

‘Serikali inachohitaji ni kuona wananchi wanapatiwa hati, wanarasimishiwa makazi yao
na kua na hakika ya usalama wa milki zao. Matarajio ya Serikali ni makubwa sana hadi
kuingia mkataba na nyie warasimishaji, alisema Kamishna komba’.

Aidha, Komba aliweka wazi kwamba, ofisi yake imepokea maagizo kutoka kwa Katibu
Mkuu wizara ya Ardhi kwamba hadi kufikia tarehe 30, Agosti mwaka huu 2020, kila
kampuni ambayo inafanya kazi ya urasimishaji katika jiji la Arusha iwe imekamilisha
kazi zake zote.

Alitoa rai kwa makampuni yote ambayo tayari yalishaingia mkataba na
wananchi kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kazi hizo vinginevyo watakuwa
na wakati mgumu kwani hata yeye amechoka kupokea malalamiko ya urasimishaji.
Katika kuhakikisha kwamba kero zote za urasimishaji zinakwamuliwa, Wizara ya Ardhi
imeunda kikosi kazi maalum kitakachosaidia kukwamua kero hizo ili makampuni hayo
yasikwame kukamilisha kazi zao kwa muda waliopewa.

Kikosi kazi hicho kinachoongozwa na Bwn. Praygod Shao amabaye ni Afisa Ardhi, kitakuwa kinapitia kazi zote zinazozalishwa na makampuni hayo ya urasimishaji na kutoa msaada wa kitaalam pale panapohitajika ili kuwaongezea kasi ya upimaji ambayo ndiyo lengo kuu la urasimishaji. Kama upimaji ukikamilika vizuri, umilikishaji hautakuwa ni tatizo kwa sababu kila mwananchi anatamani apimiwe ili amilikishwe kwa mujibu wa sheria.